November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Azania kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wanawake

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online,Mwanza

BENKI ya Azania imeihakikishia Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kuwa wamekuja kuwakomboa wanawake kutoka kwenye mikopo ya ‘kausha damu’ kwa kuja na mikopo ya riba ndogo ambayo itawawezesha kukopa fedha, kufanya shughuli zao na kupata tija.

Hayo yamesemwa leo Novemba 17, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Biashara za Serikali wa Benki ya Azania, Samson Mahimbi wakati akiwasillisha mada kwenye Mkutano Mkuu wa 40 wa ALAT unaofanyika jijini Mwanza.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Biashara za Serikali wa Benki ya Azania, Samson Mahimbi.

Mahimbi amesema Benki ya Azania inatoa mkopo wenye riba ya asilimia moja kwa mwezi, huku ikitoa mkopo kwa mwaka wenye riba ya asilimia 12 kwa mwaka, na wakati huo huo wanawake wanapokwenda kufungua akaunti ya biashara ni bure.

“Tunafahamu moja ya changamoto kubwa ya mikopo inayotolewa kwa riba za juu, ni mikopo ya kausha damu.Benki ya Azania imekuja na parkage (kifurushi) maalumu kwa ajili ya wao kukopa mikopo ya riba nafuu. Mwanamke yeyote anapokuja Benki ya Azania, kwanza atafungua akaunti bure, na makato yote ambayo alitakiwa kukatwa kila mwezi sisi tumeyatoa.

“Lakini kila anapokuja kutoa fedha kwenye akaunti ya biashara hakatwi kiasi chochote kile cha fedha, na anapochukua mkopo, riba yake ni asilimia moja tu kwa mwezi, na anapochukua mkopo kwa mwaka mkopo ni asilimia 12. Ni kwamba tumetoka kwenye mikopo ile ambayo inakopeshwa kwa asilimia 18 hadi 20, na kuja hadi asilimia 12 kwa mwaka, na asilimia moja kwa mwezi” amesema Mahimbi.

Mahimbi amesema pia wanakopesha wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wamepata mafunzo kwenye vyuo vya VETA na SIDO ambao Benki ya Azania inawakopeaha kuanzia sh. milioni nane kwa mtu mmoja ama kikundi hadi sh milioni 20. Na pia akionesha mafanikio kwa kile alichokifanya, anakopeshwa kuanzia sh milioni 20 hadi 50, na akionesha mafanikio zaidi anakopeshwa sh. milioni 50 hadi sh. milioni 200, na akiweza kutanua kazi yake, anakopeshwa sh milioni. 200 hadi 500.

Mahimbi amesema mikopo kwa Watumishi wa Umma wanakopeshwa kwa riba nafuu ambayo ipo kwenye Mfumo wa ESS, na muda wa kurudisha ni mpaka miaka 12, na riba yake ni nafuu na wezeshi.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu ALAT

Pia wanatoa mikopo ya nyumba kwa watu wote mpaka miaka 25. Na kuna aina tatu ya mikopo hiyo ya nyumba, mosi ni unenzi wa nyumba kuanzia chini mpaka juu, pili ni kumnunulia nyumba mteja, halafu akiwa analipa taratibu hadi atakapomaliza deni lake, na tatu ni ukarabati wa nyumba, ambapo benki inamuwezesha mteja kufanyia marekebisho ya nyumba, halafu atalipa taratibu.

Mahimbi amewaomba mameya, wenyeviti, na wakurugenzi wa halmashauri kuweza kuitumia Benki ya Azania kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, kwani tayari kwa sasa ina mkataba wa kukopesha madiwani.

Benki ya Azania ndiyo Mdhamini Mkuu wa Mkutano Mkuu wa 40 wa ALAT, na wamemuahidi Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, kuwa wataendelea kudhamini mkutano huo kwa miaka kadhaa ijayo.

Watumishi wa Benki ya Azania kutoka mikoa mbalimbali, wakitambulishwa kwenye Mkutano wa ALAT