January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Mambo ya ndani yajivunia kusimamia amani miaka 60 ya uhuru

Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline, Dodoma.

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara inajivunia mfanikio kadhaa ikiwemo  kusimamia jukumu kubwa la kuhakikisha Nchi ya Tanzania  na watu wake wanakuwa katika hali ya amani, utulivu na usalama.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Waziri wa Wizara hiyo,George Simbachawene ambapo amesema baada ya uhuru, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imepitia katika hatua kadhaa za mafanikio, ikiwemo  kusimamia jukumu kubwa la kuhakikisha Tanzania na watu wake wanakuwa katika hali ya amani.

Hatua hiyo imewafanya   watanzania na  wageni kuendelea kuishi katika hali ya amani, utulivu na usalama na wananchi  wakiendelea na shughuli za kiuchumi na kimaendeleo.

“Sambamba na kufanikiwa  kudhibiti matukio ya mauaji ya vikongwe, walemavu wa ngozi na uchunaji wa ngozi ya binadamu katika mikoa ya nyanda za juu kusini na mikoa ya kanda ya ziwa,”amesema Waziri Simbachawene.

Hata hivyo ameyataja Mafanikio mengine ni mabadiliko ya kimuundo kwa baadhi ya Idara zake kuwa Jeshi kamili, ambapo Kikosi cha Zimamoto kilibadilishwa na kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji kuwa Jeshi la Uhamiaji.

Akizungumzia makazi ya Polisi Waziri Simbachawene amesema umefanyika uboreshaji wa Ofisi na Makazi ya Askari wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo kwa sasa Wizara imebadilisha mfumo wa ujenzi wa nyumba za askari kutoka nyumba za mabati na kuwa za kisasa.

Amesema baada ya uhuru, Jeshi la Polisi limejenga nyumba 10,048 za makazi ya Maafisa na Askari wake katika Mikoa mbalimbali nchini.

Amesema  kati ya mwaka 2016 hadi sasa Jeshi la Magereza limejenga nyumba 310 za kisasa zenye uwezo wa kuhudumia familia 564 kwa ajili ya makazi ya Maafisa na Askari.

Kwa upande wa Idara ya Uhamiaji,Waziri huyo amesema  ina jumla ya nyumba 491 za Maafisa na Askari wake katika Mikoa mbalimbali Nchini zilizonunuliwa na kujengwa baada ya Uhuru.

Amesema Jeshi la Zimamoto limefanikiwa kujenga nyumba 95 kwa ajili ya makazi ya Maafisa na Askari katika Mikoa mbalimbali Nchini ukilinganisha na nyumba za makazi ya Askari ya kutosha familia 14 zilizokuwepo wakati wa Uhuru.

Kwenye Ujenzi wa viwanda amesema Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, (SHIMA) kupitia Ubia baina yake na PSSSF Nchini limekamilisha ujenzi wa Viwanda vinne vya utengenezaji wa bidhaa za ngozi, vinavyojengwa katika eneo la Gereza Karanga Mjini Moshi.

Aidha, kimejengwa Kiwanda cha Ushonaji cha Jeshi la Polisi Tanzania katika eneo la Kurasini Jijini Dar es Salaam, kitakapo kamilika kitakuwa na uwezo wa kushona sare 500 kwa siku ukilinganisha na kilichorithiwa toka wakoloni kinachozalisha sare 200 kwa siku.

“Kiwanda hicho hivi sasa kinatengeneza “crown’, kushona vyeo mbalimbali vya askari “rank and file’ na kuokoa fedha zilizokuwa zikitumika kuagiza nje,”amesema.

Aidha Idara ya Uhamiaji 2021 imeanzisha Kiwanda kidogo cha Ushonaji wa nguo na Sare mbalimbali za askari na Maafisa wa Uhamiaji, lengo likiwa ni kutosheleza mahitaji ya ushonaji wa sare za askari na Maafisa kiwandani hapo badala ya kupeleka kwenye viwanda ambayo gharama zake ni kubwa.

Amesema Idara ya Uhamiaji imeendelea kuboresha Kiwanda chake cha Uchapaji Kijichi (KPU-Kijichi Printing Unit) kilicho nunuliwa mwaka 2001 kutoka Benki ya Taifa ya Kibiashara (NBC) kwa ajili ya kuchapa nyaraka mbalimbali za Idara ya Uhamiaji ambazo zimekuwa zikitumika tangu baada ya Uhuru hadi sasa.

“Kuwepo kwa kiwanda hicho kumepunguza gharama za uchapaji wa nyaraka nje ya Idara na pia imesaidia kulinda usalama wa nyaraka zake,”amesema

Aidha kwa sasa Idara ina lengo la kuwezesha kiwanda hicho kujiendesha kibiashara ili kutimiza maelekezo ya Serikali kuwa kila taasi ya Kijeshi iwe na miradi inaingiza faida.