April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya madini kushiriki jukwaa la biashara Uingereza

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

TIMU ya Wataalam wa Wizara ya Madini ikiongozwa na Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, inatarajia kushiriki katika Jukwaa Maalum la Biashara kati ya Tanzania na Uingereza.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa Sekta ya Madini kwenye jukwaa hilo, Katibu Mkuu Mahimbali amesema Wizara inatarajia kufanya wasilisho maalum litakalotoa wasaa wa kueleza fursa za kiuwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini nchini hususan kwenye madini muhimu na mkakati.

Wataalam kutoka Wizara hiyo ni sehemu ya ujumbe maalum wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki jukwaa hilo lililoanza Novemba 20, 2023 jijini London ambao pia linahusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania.

Aidha, Mahimbali ameongeza kuwa, Wizara inatarajia kufanya mkutano na Taasisi ya Jiolojia nchini Uingereza ambao unalenga kuimarisha uhusiano na maeneo mapya ya ushirikiano na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

‘’Tutakutana na Kampuni nchini Uingereza zenye nia ya kuwekeza Tanzania, pia tutashiriki kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania tulioambatana nao na wafanyabiashara wa Uingereza hususan wenye nia ya kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani madini,’ amesema Mahimbali.

Wizara ya Madini inaendelea kutekeleza mikakati yake ikiwemo moja ya vipaumbele vyake vya kuendeleza madini muhimu na mkakati ambapo katika Mwaka wa Fedha 2023/24, wizara imepanga kutekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya utafiti na kutangaza fursa za kiuwekezaji zilizopo.

Kuhamasisha uwekezaji katika utafutaji uchimbaji wa madini mkakati na madini muhimu, kutoa leseni na kuandaa Mpango Mkakati wa uendelezaji wa shughuli za uchimbaji wa madini nchini.

Aidha, kupitia Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri kupitia GST, Wizara inapanga kufanya utafiti wa kina kwa njia ya ndege (Geophysical Airborne Survey) angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Kimsingi, taarifa za utafiti ndizo zinazoshawishi uwepo wa uwekezaji na hivyo kuwezesha uwekezaji wa uhakika.

Kufuatia umuhimu wa Sekta ya madini katika maendeleo ya kiuchumi na kufuatia umuhimu wa jukwaa hilo kwa sekta, Mahimbali ametoa wito kwa wadau na watu wengine waliopo nchini humo wenye nia ya kuzungumza na timu ya wizara kuweza kufanya hivyo.

“Tungepata maoni mbalimbali hususan ndugu zetu Diaspora ili tubadlishane mawazo na ujuzi utakaosaidia kuleta mabadiliko nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla katika mnyororo mzima wa thamani madini,”,amesisitiza Mahimbali.

Kutokana na umuhimu wa jukwaa hilo kwa sekta ya madini, Mahimbali ametoa pongezi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida kwa kuandaa ujumbe wa Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ukiongozwa na Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na kampuni ya Clyde & Co Tanzania iliyoshiriki kuratibu ujumbe wa Tanzania nchini humo.