January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Elimu kusaidia kazi za wabunifu DIT

Na Grace Gurisha, TimesMajira Online

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amesema Wizara hiyo itasaidia kazi za ubunifu zinazofanya na wanafunzi na wakufunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kutoka kwenye maonesho na kwenda kutatua changamoto katika jamii.

Profesa Mdoe ametoa ahadi hiyo leo baada ya kumaliza kutembelea banda la Chuo hicho katika maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanaondelea Mkoani Dar es Salaam.

Amesema, ameona vitu vya aina mbalimbali, kazi za wanafunzi na kazi za wabunifu wakufunzi na kuzungumza nao kutaka kujua wamefikia hatua gani kwenye bunifu zao kwa sababu kuna baadhi ya kazi alishaziona awali.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe akipewa maelekezo ya mchanga mzuri ambao unaweza kutumika kwenye ujenzi wa nyumba kutokana na utafiti uliyofanywa

“Ningependa kazi zenu kwa sasa zitoke kwenye maonesho zifike hatua ya kwenda kutatua changamoto kwenye jamii, mfano kuna binti amebuni kifaa kwa ajili ya watoto njiti basi kifaa hicho kifike hospitalini,” amesema Profesa Mdoe

Amesema wao kama wizara watachukua changamoto za taasisi hiyo ili vifaa vilivyobuniwa viweze kuondoka kwenye hatua ambavyo vipo, vifike hatua vikatatue changamoto ambazo zinapaswa kutatuliwa.

Naibu Katibu huyo, amesema DIT ni mahali ambapo kuna mafunzo mazuri yanafanyika, mafunzo yao ni ya mfumo wa kujifunza viwandani, kwa sababu mafunzo yao yameunganishwa moja kwa moja viwandani.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe akipewa maelekezo na ubunifu wa kifaa cha kuwafundishia madaktari.

Akizungumzia masula ya ubunifu, amesema kuna sehemu wanaita atamizi ni mahali ambapo mbunifu mwenye wazo lake anaweza kwenda pale akawekewa mazingira ya kuweza kulifanyia kazi kufika kwenye huduma au bidhaa.

“Nina matumaini muda si mrefu tutaanza kupata matunda mazuri  kutoka kwenye zile atamizi, kwa hiyo niwaambie wabunifu hasa waliyokuwepo Dar es Salaam ni rahisi kufika DIT wakajiandikisha na kupeleka mawazo yao, ambapo watawekewa mazingira wezeshi hata nayo wa zaidi wao pamoja na jamii kwa ujumla, ” amesema Profesa Mdoe 

Aidha, ameitaka tasisi hiyo kuendelea kujitangaza ili iweze kupata wanafunzi wengi kwenye programu za ‘masters’ kwa sababu wanafunzi  ni wachache, lakini kuna watu wanauhitaji wa kufika katika hatua hiyo.