Na Doreen Aloyce, Timesmajira online, Dodoma
Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji imewakutanisha Makatibu Tawala wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuwapitisha juu ya muongozo utakao rahisisha utendaji kazi wa majukumu yao kwenye ngazi ya Halmashauri na Mkoa katika sekta inayosimamiwa na Wizara hiyo.
Hiyo ikiwa ni jitihada za serikali katika kuhamasisha, kuhakikisha na kuweka mazingira bora ya kufanya biashara,uwekezaji na viwanda kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini.
Akifungua warsha hiyo ya siku mbili Jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu,Mkurugenzi wa Idara ya uwezeshaji kiuchumi na maendeleo ya sekta binafsi kutoka Wizara ya Biashara, Uwekezaji na Viwanda Conrad Milinga amesema kuwa Wizara imeona kuna haja ya kushirikiana na Wizara ya Tamisemi kuanzisha idara ambayo itasaidia kufanikisha malengo ya Rais Samia Suluhu Hassani katika sekta inayosimamiwa na Wizara hiyo.
Milinga amesema,adhima ya serikali ni kujaribu kuweka mazingira mazuri kuanzia ngazi ya chini ambapo awali hapakuwa na watekelezaji hivyo ikaona kuna haja kwa kushirikiana na Wizara ya Tamisemi kuanzisha idara hiyo kuanzia ngazi ya Halmashauri mpaka Mkoa.
“Rais anapoleta wawekezaji akute watekelezaji kwani awali hapakuwa na maelewano mazuri baina ya Serikali na Serikali,ninyi ni timu tunategemea muwe vielelezo vizuri,mtakuwa na kazi ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara ya namna ya kufanya biashara zao kwa ufanisi kujua wapi anapaswa kuanzia kabla ya kusajili biashara zao kwa kufanya hivyo tutakusanya mapato mengi kwa amani na kujenga mahusiano mema tunaamini hamtatuangusha “amesema Milinga.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara wa Wizara hiyo Sempeho Nyari amesema kuwa lengo la kuwaita watendaji hao ni kuwaelewesha na kuhamasisha ujengaji wa mazingira wezeshi ya kibiashara,uwekezaji na viwanda.
Amesema kuwa katika kuboresha mazingira ya biashara serikali imetengeneza idara mpya chini ya Wizara ya Tamisemi katika ngazi ya mikoa na halmashauri kwa lengo la kufanya kazi kwa ufanisi na kutaka kuondoa vitu vyote vinavyo sababisha kikwazo na kuwakwaza wafanyabiashara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa warsha hiyo akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Sangu Deogratias wamesema kuwa wanaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuanzisha idara hiyo ili kazi za viwanda ziweze kufanyika kuanzia wizarani mpaka chini kwani utekelezaji wa chini haukuwa na usimamizi .
“Kupitia vikao kama hivi vinatusaidia kuwa na mtazamo mzuri wa kufanya kazi karibu na hawa wafanyabiashara wanaolipa kodi na tunaiahidi serikali hatuta waangusha “amesema Sangu.
Nae Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mororgoro Beatrice Charles,amesema kuwa muongozo huo unaenda kuwasaidia kufanya kazi kwa weledi na kwamba wataenda kuondoa vikwazo eneo la uwekezaji na ujenzi wa viwanda itakayosaidia kuongeza mapato.
“Lakini pia tutaenda kuimarisha mahusiano kati ya mikoa, halmashauri pamoja na sekta binafsi zilizopo katika maeneo yetu,tutaweka nguvu kwa makundi yote kuwapa ushauri ili wafanye biashara zao vizuri jambo ambalo litasaidia kukuza sekta binafsi,”amesema Beatrice.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato