January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisema jambo kwenye kikao kazi cha maandalizi ya mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito kilichofanyika leo Jijini Dodoma

Wizara ya Afya kuja na mfumo wa ufuatiliaji wajawazito nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Dodoma

WIZARA ya Afya inatarajia kuja na mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito wote toka wanapofika kliniki kwa mara ya kwanza hadi baada ya siku 42 za kujifungua.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima leo alipokutana na wataalam wa afya katika kikaokazi cha maandalizi ya utengenezaji wa mfumo huo.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale akisema jambo kwenye kikao kazi cha maandalizi ya mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito kilichofanyika leo Jijini Dodoma.

“Nataka muwe mnafuatilia taarifa za wajawazito na kujua maendeleo yao toka wanapofika kituoni siku ya kwanza mpaka baada ya kujifungua kwa data za kila siku na kujua kwa namna gani wajawazito au mama baada ya kujifungua ameweza kupata huduma zetu na muweze kuchukua hatua pale mnapoona changamoto” amesema Dkt. Dorothy Gwajima.

Waziri Gwajima amesema kuwa ili kuweza kuwa na mfumo wenye ufanisi ni lazima tusisitize matumizi sahihi ya takwimu na kuwataka wataalam wa afya katika kazi zao kuhakikisha wanachukua takwimu zote zinazohitajika kwa ajili ya matuzimu katika mfumo huo.

Waziri Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali katika kupambana na vifo vya wajawazito imefanya mambo mengi ikiwemo kuanzisha Kampeni maalum ya Jiongenze Tuwavushe Salama iliyoanzishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kupunguza na kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.

“Serikali imejenga vituo vingi vya huduma ngazi zote na mwamko wa wajawazito wanaojitokeza kuhudhuria kliniki umekuwa mkubwa” amesema Dkt. Dorothy Gwajima na kuongezea kuwa bado elimu inahitajika kutolewa kwa ili wajawazito wafike katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuanza kliniki mapema.

Washiriki wa kikao kazi cha maandalizi ya mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito kilichofanyika leo Jijini Dodoma

“Sasa hivi mwitikio umeongezeka, wajawazito wanajitokeza na kujifungua katika vituo vya kutolea huduma kati yao wengine wanafariki, lakini tukijadili kujua kwanini amefariki na tukifuatilia wakati alipokuwa kliniki tunagundua hatukumfuatilia vizuri, hiki ndio kitu tunachoimarisha ili ufuatiliaji uwe imara” amefafanua Dkt. Dorothy Gwajima.

Waziri Gwajima amesema kuwa katika kuimarisha mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa taarifa za wajawazito, wanatarajia kuimarisha ufuatiliaji wa mteja mmoja mmoja toka anapopata ujauzito, muda wa kuanza kliniki, kujifungua mpaka baada ya siku 42.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale amesema kuwa kwa kupitia kanzidata wanazochukua kutoka kwenye taarifa za wajawazito zinawasadia kujua bidhaa gani za dawa zinazihitajika kumhudumia mjamzito, miundombinu ipi wanahitaji, inaonyesha uwajibikaji wa watumishi wa afya kwa ujumla wao na mmoja mmoja, pamoja na kutuonyesha kama miongozi iliyopo inatija katika kusaidia kutoa huduma bora kwa wajawazito.

“Hakuna njia nyingine ambayo tutaitumia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi zaidi ya kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa mama mmoja mmoja kama kanzidata hii inavyotaka” amesema Dkt. Sichwale