January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Afya kuadhimisha kilele magonjwa yasiyopewa kipaumbele Januari 30

Mwandishi wetu, Timesmajira

TANZANIA kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuadhimisha siku ya kilele cha magonjwa yasiyopewa kipaumbele ambapo kwa mwaka huu yanatarajiwa kuadhimishwa Januari 30 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam na Ofisa Programu kutoka Wizara ya Afya katika mpango wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Issac Njau wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo yaliondaliwa na Wizara hiyo chini ya Mpango wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele.

Amesema maadhimisho hayo yatabebwa na kauli mbiu ya ‘Tuungane tuchukue hatua tutokemeze magonjwa yasiyopewa kipaumbele’ na yanatarajiwa kufanyika katika ngazi ya mikoa pamoja na Halmashauri kwa kutoa elimu na hamasa ya magonjwa hayo kwa jamii.

“Tunaadhimisha tofauti na mwaka uliopita mwaka huu tutatoa elimu katika ngazi ya mikoa pamoja na Halmashauri juu ya magonjwa haya yasiyopewa kipaumbele,”amesema.

Amesema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kutoa elimu kwa jamii ili iweze kupata uelewa pamoja na taasisi mbalimbali na Serikali kwa ujumla iweze kuchukua hatua ya pamoja na kuungana kutokomeza magonjwa hayo.

Kwa upande Dkt. Clara Mwansasu ambaye pia ni Ofisa Programu wa kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya amesema Tanzania imekuwa na magonjwa hayo yasiyopewa kipaumbele na imekuwa ikipambana nayo kwa njia ya kinga tiba.

Amesema baada ya kufanya tathimini kati ya mwaka 2006 hadi 2015 yalikuwa yakionekana kuathiri maeneo makubwa .

“Tunafanya tathimini kila baada ya miaka mitano ya kuwezesha dawa mara moja kwa mwaka kwa lengo la kuangalia hali ya ugonjwa ambapo kwa sasa hivi ugonjwa wa matende na mabusha umeshuka kutoka Halmashauri 119 za awali mwaka 2006 tulipoanza programu hadi tulipofikia 2023 tumebaki katika Halmashauri saba tu,”amesema.

Kwa upande wa ugonjwa wa trakoma Dkt. Mwansasu amesema walianza na
Halmashauri 71 zilizokua na maambukizi ya hali ya juu ya ugonjwa hu baada
ya kutoa kingatiba ya Zithromax, ulipungua hadi halmashauri 9 tu ambazo ni Longido, Kiteto, Kalambo, Simanjiro, Ngorongoro, Mpwapwa, Kongwa,
Chamwino na Monduli.

Amesema ili kujikinga na ugonjwa wa trakoma au vikope mtu anapaswa kumeza kingatiba ya kuzuia ugonjwa huo kila inapotolewa kwenye jamii,kusafisha uso mara kwa mara, kuhakikisha uso wa mtoto hauna makamasi, matongotongo, na mabaki ya chakula, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara.

Pia kujenga na kutumia choo kwa usahihi,kufanya usafi wa mazingira ili kupunguza mazalia na kuvutia nzi pamoja na kuepuka kuchangia leso, taulo au nguo zingine kujifutia usoni.

Kwa upande wa ugonjwa wa kichocho na minyoo tumbo amesema unatibika na vidonge vya Praziquantel lakini madhara ya ugonjwa wa kichocho yanahitaji matibabu mengine zaidi.

Amesema mtu mwenye dalili za ugonjwa wa kichocho, anashauriwa kwenda kituo cha huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kwa ujumla walio katika maneno yalioathirika zaidi na magonjwa hayo waweze kushiriki katika umezaji wa dawa tiba ili hatua ziweze kuchukuliwa zaidi.