November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara, NHIF zapewa’rungu’ Kitita kipya

Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline,Dar

KAMATI ya Kupitia Kitita cha Mafao ya NHIF 2023 imetoa msimamo wa kitaalam kwa kuitaa Wizara ya Afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) iendelee na utekelezaji wa Kitita cha mafao kilichoboreshwa cha NHIF cha mwaka 2023 kama ilivyoshauliwa na Kamati.

Uamuzi huo umetangazwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati, Dkt. Baghayo Saqware, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho ya kitita hicho cha mwaka 2023.

Amesema kufuatia matamko yaliyotolewa na Watoa Huduma za Afya wa Sekta Binafsi (APHFTA) ya kupinga Kitita hicho, Kamati inatoa msimamo wake wa kitaalam kwamba Wizara kupitia NHIF iendelee na utekelezaji wa Kitita cha mafao kilichoboreshwa.

Amesema, lazima ieleweke kwamba Kamati hiyo iliundwa na Waziri wa Afya kwa ajili ya kumshauri masuala ya kitaalamu kuhusu namna bora ya kuandaa na kutekelezeza kitita cha mafao kilichoboreshwa cha mwaka 2023.

Alisema matokeo ya uchambuzi uliofanywa na Kamati kwa kuzingatia vigezo vya uchambuzi vya Kamati na katika kuhakikisha Mfuko unaendelea kuwa stahimilivu, Kamati imefanya maboresho katika kitita cha mfao cha mwaka 2023 ambapo matokeo ni kama ifuatavyo;

Moja, Kati ya dawa 722 kama zilivyobainishwa katika kitita cha mafao cha mwaka 2023, bei ya dawa 237 zimeongezeka, bei ya dawa 239 zimepungua na 246 zimebaki kama zilivyopendekezwa awali;

Mbili, katika huduma za upasuaji na vipimo baadhi ya bei za huduma
zimepungua, kuongezeka na kubaki kama ilivvyopendekeza awali.

Tatu, amesema Katika viwango vya ada ya ushauri na kumuona daktari ikilinganishwa na mapendekezo yaliyowasilishwa katika kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023, baadhi ya ada kwa kuzingatia ngazi ya aina ya utaalam viwango vimeongezeka, vimepungua na baadhi kubaki kama ilivyokuwa awali.

“Endapo Mfuko ungelipa madai kwa kutumia mahudhurio ya mwaka 2022-23 kwa kuzingatia bei iliyopendekezwa na Mfuko katika kitita cha 2023, madai ya sh. bilioni 585.07 yangelipwa sawa na punguzo la asilimia 17 ikilinganishwa na kitita cha mwaka 2016,” amesema.

Aidha, amesema endapo mapendekezo ya bei ya Kamati yatatumika Mfuko utalipa kiasi cha sh. bilioni 577.45 sawa na punguzo la
asilimia 18 ikilinganishwa na kitita cha mwaka 2016.

Dkt. Saqware, amesema Mapendekezo ya Kamati ya Wataalam ni pamoja kuanza kutumika kwa Kitita cha Mafao cha mwaka 2023 pamoja na
maboresho yaliyopendekezwa na kamati katika sehemu ya ada ya
ushauri na kumuona daktari, huduma za dawa, upasuaji na vipimo.

Mengine ni Kitita cha mafao cha NHIF kifanyiwe mapitio ya bei za huduma kila baada ya miaka miwili ili kuwezesha mabadiliko ya bei kuzingatiwa kwa wakati kama inavyotekelezwa na taasisi mbalimbali kama vile Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Kitita hicho kwa wanufaika NHIF utekelezaji wake unaanza rasmi leo, ambapo juzi Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, aliwahakikishia wanachama kwamba hakuna atakayekosa huduma.