Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dar
WIZARA ya Mifugo na Ufuvi ina mpango wa kuunda mamlaka itakayoratibu na kusimamia malisho ya mifugo na kuyatafutia masoko na mazao yanayotokana na sekta ya mifugo.
Mpango huo umetangazwa wiki hii jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki,kwenye mkutano wa wadau wa mifugo.
Amesema Serikali inajali maslahi ya wafugaji na kwamba itatekeleza mawazo ya wadau wa sekta ya mifugo katika kuboresha sekta hiyo na kutengeneza mazingira bora ya ufugaji ili sekta hiyo iendelee kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Waziri Ndaki amesema Serikali inafikiria kuanzisha mamlaka itakayosimamia malisho na masoko ya mifugo na mazao yake na kubainisha kuwa mamlaka hiyo itafanya bidii kuinua sekta hiyo pamoja, kupunguza migogoro na kuhamahama kwa wafugaji.
“Serikali itaunda mamlaka hii na moja ya jukumu lake kubwa ni kuaangazia malisho na kutafuta masoko ya mazao ya sekta hii ya mifugo,” amesema Waziri Ndaki.
Ametumia mkutano huo huo kuwahakikishia wafugaji kuwa Serikali ipo na itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wafugaji kwa kuwa inatambua mchango wao katika maendeleo uchumi wa taifa pamoja na kutengeza ajira kwa vijana.
Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa TADB, Mzee Kilele, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amewahakikishia wadau wa sekta ya ufugaji ushirikianao kutoka TADB na kueleza kwamba mikutano yenye malengo mazuri kama huo, inaipa benki yao fursa ya kujua, kutambua na kuona jinsi gani inaweza kuwafikia wafugaji wengi zaidi ili waweze kunufaika na fursa zitolewazo na benki hiyo.
“Hii imekua fursa nzuri kwetu kuwepo hapa. Mkutano huu unatoa nafasi kwetu kukutana na wadau wa sekta ya mifugo na na chukua fursa hii kuwahikishia kuwa benki itaendelea kuongeza kasi katika kutoa mikopo pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ili kuifanya sekta hii kuwa sekta imara yenye kuleta tija kwa wafugaji wenyewe na katika kuinua uchumi wa taifa”, amesema Kilele.
Ameeleza kuwa hadi Agosti mwaka huu, benki hiyo imetoa mikopo ya moja kwa moja kwenye sekta ya mifugo yenye thamani ya sh. bilioni 23.8 na fedha hiyo imewezesha AMCOs tano kupata ng`ombe wa kisasa na kunufaisha wafugaji 128.
Aidha, Kilele amesema benki imetoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 11.8 na fedha hiyo imewezesha ujenzi wa viwanda vinne vya maziwa.
“Kwa kutambua umuhimu wa sekta hii na uhusiano mkubwa wa baina ya sekta ya mifugo na maziwa tuliona ni vyema tutoe mikopo ambayo iliwezesha ujenzi wa viwanda vinne vya maziwa na wafugaji zaidi ya 6,000 wanauza maziwa yao kwenye viwanda hivyo,” amesema Kilele.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji Wilaya ya Karagwe, Jackson Kamkoto, amesema ukosefu wa elimu kwa wafugaji, uhaba wa maofisa ugani, uhaba wa malisho na maji zimekuwa changamoto kubwa zinazowakabili wafugaji nchini na kupendekeza Serikali kuunda chombo maalamu kitakachoratibu masuala hayo ili kuongeza tija kwenye sekta ya ufugaji.
Akifungua mkutano huo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushiriki kikamilifu katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati