November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wito watolewa kwa waendesha pikipiki

Na Judith Ferdinand, Mwanza

Wito umetolewa kwa waendesha pikipiki Mkoa wa Mwanza kufanya kazi kwa kuzingatia na kutii sheria za usalama barabarani,ili kudhibiti ajali.

Hayo yamezungumzwa na Kamanda wa Usalama barabarani Mkoa wa Mwanza (RTO) Joyce Kotecha,wakati akizungumza kwenye halfa ya kuwaapusha viongozi wa Chama cha waendesha pikipiki(UWP)Mkoa wa Mwanza, uliofanyika mkoani hapa.

Kotecha ,amesema Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda sana waendesha bodaboda,lakini anawataka wazingatie sheria ambapo wamewafanyiwa punguzo la faini hivyo wazingatie sheria na watakuwa tumepunguza ajali kwa kiasi kikubwa.

Amesema,jukumu la viongozi wa UWP ni kuhakikisha wananchi na madereva wana vaa kofia ngumu na wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kuokoa maisha ya wananchi.

“Jukumu lenu nyie viongozi kuhakikisha mnasimamia vituo vyenu,mnavitambua mnawasajili bodaboda na kuhakikisha kila mtu anavaa kofia ngumu abiria pamoja na dereva,na asiye vaa kofia muelimisha ni lazima avae kofia na asiye vaa kofia usimbebe,” amesema Kotecha na kuongeza

“Mkoa wa Mwanza mwakani tunakuwa wenyeji wa maadhimisho ya usalama barabarani kitaifa ambayo yatafanyika hapa,basi ni vizuri kufikia siku hiyo tukutwe ajali ni chache na watu wote wapo hai na tuna tii sheria za barabarani,”.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UWP Mkoa wa Mwanza Joseph Lusendamula,amesema
Wizi wa pikipiki bado ni janga linalowaandama madereva wa bodaboda kwani kuna matukio mengi yanayowakabili ya wizi wa pikipiki ambayo yanasababisha hadi vifo.

Kwa kushirikiana na serikali pamoja wanaweza kumaliza changamoto hiyo,lakini kwenye mipango mikakati yao ni kuhakikisha kunakuwa na amani.

Pia amesema ili kumaliza changamoto ya ajali za bodaboda,wamejipanga kupeleka mafunzo ya udereva wa bodaboda kwenye Mkoa mzima.

“Mafunzo hayo ni mpango mkakati awamu ya kwanza wa muda mfupi huku
mpango mkakati wa muda mrefu tutajenga chuo cha mafunzo ya udereva kwa Mkoa wa Mwanza,ambapo tutaweza kutoa mafunzo na kufundishana wenyewe hivyo kurahisisha na kusaidia mapato ya chama,” amesema.

Pia amesema,wameingia mkataba na benki ya NMB ambayo inawafadhili mafunzo pamoja na leseni kisha wanalipia taratibu,ambapo wamefanya zoezi hilo kwa Wilaya ya Nyamagana lakini litakuwa zoezi endelevu la wilaya hadi Wilaya.

Mwisho wa siku wanamatumaini kuwa madereva wao watakuwa na leseni zitakazosaidia kufanya kazi kwa kuzingitia Sheria.

Katibu Mkuu wa Chama cha waendesha pikipiki Mkoa wa Mwanza (UWP) Joseph Lusendamula, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kaa halfa ya kuwaapisha viongozi wapya wa chama hicho uliofanyika mkoani Mwanza.
Baadhi ya wana Chama cha waendesha pikipiki Mkoa wa Mwanza (UWP) waliohudhuria halfa ya kuwaapisha viongozi wapya wa chama hicho uliofanyika mkoani Mwanza. picha na Judith Ferdinand