December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wito umetolewa kwa wazee kuchanja chanjo ya UVIKO-19

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

MLIPUKO wa ugonjwa wa uviko-19, wakati umeripotiwa unaingia nchini miongoni mwa makundi yaliyokuwa katika hatari ya kuathirika dhidi ya ugonjwa huo ni wazee na wenye matatizo ya mfumo wa upumuaji.

Pia serikali katika kupambana na Uviko-19 iliendelea na jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya namna ya kujingika na ugonjwa huo pamoja na kuruhusu uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19 huku miongoni mwa makundi yaliyopewa kipaumbele kupata chanjo hiyo ni pamoja na kundi la wazee.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na timesmajira baadhi ya wazee wilayani Ilemela,wameeleza namna walivyokuwa na hofu awali lakini walipata matumaini baada ya serikali kuanza kutoa chanjo ya uviko-19.

Mmoja wa wazee hao kutoka Kata ya Nyakato wilayani Ilemela Transisi Balizukwa, ameeleza kuhusu chanjo kuwa hazikuanza sasa hivi
bali kuna chanjo ya kifua kikuu,polio na surua ambayo walichanja kipindi cha nyuma wala hazikuwa na madhara na yeye akiwa ni miongoni mwa waliopata chanjo.

“Chanjo ni kitu cha kawaida hivyo elimu inabidi itolewe zaidi maana mtu anakuambia nikichanja sito kufa,kufa ni wajibu utakufa tu ila chanjo ni tahadhari ya magonjwa,” ameeleza Balizukwa na kuongeza kuwa

“Ukweli wazee tulikuwa na hofu baada ya corona kuingia nchini na baada ya kupatikana kwa chanjo ya ugonjwa huo hofu imeondoka ikizingatiwa hadi sasa hatujasikia mtu aliyepata madhara kutokana na chanjo hiyo hivyo wito kwa wazee na jamii ikubali kuchanjwa chanjo hiyo ya uviko-19,”.

Mzee mwingine kutoka Kata ya Buzuruga Kaskazini wilayani Ilemela Amina Said,ameeleza kuwa yeye amepata chanjo ya uviko-19 na hakupata shida yoyote wala mabadiliko ya mwili.

Hivyo amewashauri wazee wengine wakubaliane na hilo la chanjo ili kuepuka maradhi kwani afikirii kama kuna watu ambao hawajapata elimu kuhusu chanjo ya uviko-19 lakini ni dharau tu.

“Hakuna mtu ambaye ajaona kwenye runinga, kusikiliza redioni,kwenye vituo vya afya sema ni imani na mitazamo potofu ya kuwa wakichanjwa watakufa……,ni kazi ngumu mpaka kuelimisha jamii hivyo Serikali iitishe vikao vya mara kwa mara kupitia serikali za mitaa ili jamii ipate elimu zaidi,”ameeleza Amina.

Mzee kutoka Kata ya Kirumba Pili Hassan,ametoa wito kwa wazee wengine na jamii kwa ujumla wajitokeze kuchanja kwani chanjo hazina madhara ata awali tulichajwa chanjo ya ndui na nyingine lakini hawakupata madhara yoyote.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mohamed Yusuph, ameeleza kuwa wazee ni wachache ambao wamejitokeza kuchanja lakini yeye ni miongoni mwa wazee waliojitokeza kuchanga chanjo hiyo ya uviko-19.

Ameeleza kuwa kunachagamoto kwa baadhi ya wazee ambao wanakaririshwa na wengine
wanachukulia kama mambo ya mila hivyo wanaenda kuchanja kwa kujificha wakihofia kuwa familia ikijua itamsema na wengine wanawashilikisha watoto wao ambao wanawakataza wasichanje.

“Wito kwa wazee wenzangu wajitahidi wanapoamua kuchanja chanjo ya uviko-19 aamue mwenyewe,maana akifuata ushauri wa watu wengine watajikuta wanashindwa kupata chanjo hiyo kwa ajili ya kinga dhidi ya corona na ikizingatiwa ni moja ya kundi ambalo lipo kwenye hatari,”ameeleza Yusuph.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea Haki za Wazee (MAPERECE) Magu Julius Mwengela, ameeleza kuwa wamekuwa na kampeni kubwa ya kuhakikisha wazee wanapata elimu kuhusiana na uviko-19 na kisha wanapata chanjo.

Mwengela ameeleza kuwa maeneo yote ya vijiji ambayo wanahamasisha wanategemea Baraza la Wazee ambalo lina wazee wenyewe,vijana na wanawake ambapo wameunda kamati za ufuatiliaji wa chanjo hiyo kwa kushirikiana na wahudumu afya ngazi ya jamii.

Amesema lengo ni kumnusuru mzee asiweze kupata maambukizi mapya na athari za Uviko-19,hivyo wanatoa elimu kwa kupitia nyumba kwa nyumba,midahalo na mikutano hali ambayo imesaidia wazee kwenda vituo vya afya kuchanjwa.

Ameeleza kuwa kiuhalisia wazee wengi hawana taarifa hususani wa maeneo ya vijijini kwani hawana, redio,runinga wala simu za mkononi ambayo ujumbe mara kwa mara unatumwa unaoeleza namna ya kujikinga,elimu ya chanjo ya uviko-19 na kuhamasisha watu kuchanja.

“Kwa ajili ya kujikinga na pia kupata chanjo hiyo ya uviko-19,tukaamua wazee waweze kupata elimu hii ili iweze kuwasaidia kujua kuna nini kinachoendelea kwenye dunia na wasije kupoteza uhai wao kwa sababu ya kutokujua lakini kwa kufanya hivi kwa sababu tunashughulika na masuala ya wazee,ambapo tumefanya katika Wilaya za Mwanza ikiwemo Magu,Kwimba, Misungwi na Sengerema,”ameeleza Mwengela.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Ilemela Mohamed Yusuph, akizungumza wakati Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula alipo na wazee wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa ajili ya kuwapa elimu juu ya kuhamasisha sensa na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kilichofanyika wilayani hapo.(picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya wazee walikutana na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula kwa ajili ya kupewa elimu juu ya kuhamasisha sensa na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kilichofanyika wilayani hapo.(picha na Judith Ferdinand)