November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wito kwa wanahabari kuandika habari zinazohusu bima

Judith Ferdinand, Mwanza

Wito umetolewa kwa waandishi wa habari kuandika habari zinazohusiana na masuala ya bima ili kukuza sekta ya bima pamoja na uelewa katika jamii.

Kwani masuala ya bima bado hayapewi kipaumbele katika jamii huku uelewa juu ya bima ukiwa bado ni mdogo kwa watanzania walio wengi.

Wito huo umetolewa na Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Bima Tanzania, Khadija Issa Said,wakati akifungua mafunzo ya bima kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza,yalio andaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa.

Khadija amesema,wanatambua bado kuna changamoto katika kuzifikia huduma za bima,matumaini yao ni kuwa wanahabari wakiamua wanaweza kuikuza sekta ya bima na kuwaokoa wananchi dhidi ya majanga mbalimbali.

“Tunajua masuala ya bima bado hayapewi msukumo mkubwa katika jamii zetu,tunatambua kwamba uelewa wa bima bado ni mdogo kwa watanzania wengi,tunaona mnavyoweza kuandika makala na taarifa mbalimbali za miradi,hivyo sasa mjikite kutoa elimu ya bima kwa jamii ikiwemo wafanyabiashara,machinga na wengine wote hao wanahitaji kuwa na Kinga za bima dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo ya moto,ajali na maradhi,”amesema Khadija.

Kwa upande wake Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa Sharif Ali Hamad, amesema sababu ya kutoa elimu hiyo kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uelewa wa bima ili kuwa rahisi kwao kufikisha elimu ya bima kwa jamii.

Amewaomba waandishi waelimishe jamii ili waweze kuwa na bima ambayo itawasaidia kupata huduma mfano mtu akiugua anachukua kadi anaenda kutibiwa hivyo ina mrahisishia upatikanaji wa huduma.

“Jamii yetu sasa hivi imekabiliwa na majanga mengi,kama vile ajali,moto kwenye masoko,shule za bweni,viwanda hata kwenye nyumba za makazi,majanga haya yanapotokea yanasababisha kupoteza maisha ya watu na kupoteza mali nyingi,kuna umuhimu wa kupeleka elimu ya bima katika jamii,” amesema Sharif.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko amesema vyombo vya habari vina nafasi katika kuelimisha jamii juu ya suala la bima.

“Sisi waandishi wa habari wa Mwanza kupitia MPC tunaamini suala la bima ni mtambuka,msiwachukulie waandishi wa habari kama daraja la kufikisha ujumbe lakini pia nao wawe sehemu ya kunufaika na bima wao itawasaidia kwani wanaendesha vyombo vya moto,afya pia tuliingie makubaliano na NHIF),”amesema Soko.

Hivyo alitoa ombi kwa Waziri wa Habari asimamie usalama wa waandishi wa habari hasa katika kipengele cha bima liwe jambo la kwanza.

Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa Sharif Ali Hamad, akizungumza katika mafunzo ya bima kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza,yalioandaliwa na TIRA Kanda ya Ziwa. Picha na Judith Ferdinand
Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko akizungumza wakati akifungua mafunzo ya bima kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza,yalioandaliwa na TIRA Kanda ya Ziwa. Picha na Judith Ferdinand
Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Bima Tanzania Khadija Issa Said akizungumza wakati akifungua mafunzo ya bima kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza,yalioandaliwa na TIRA Kanda ya Ziwa. Picha na Judith Ferdinand