Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Wito umetolewa kwa waandishi wa habari kuandika habari kwa kuzingatia weledi wa taaluma ya uandishi wa habari pamoja na kutumia fursa ya mitandao kuhabarisha jamii habari zenye uhakika.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko, wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari kwa ngazi ya Mkoa yalioandaliwa na taasisi ya Internews Tanzania kwa kushiriki na MPC yaliofanyika mkoani hapa ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti”.
Soko amesema,wanafahamu kuwa wanahama kutoka kwenye uandishi ule waliozoea na wanakwenda kwenye uandishi wa majukwaa ya kidigitali zaidi na huko kuna changamoto zake.
Hivyo ujio wa mitandao ya kijamii isiwafanye waandishi wa habari kusahau maadili bali wafanye kazi kwa kuzingatia weledi na wanapofanya kazi wazichakate na kuzingatia misingi ya uandishi wa habari.
Amesema waandishi wafanye kazi kwa weledi na kwenye mipaka wazingatie mipaka,kuweka uzalendo mbele na misingi ya uandishi wa habari.
“Niwasihi ndugu zangu waandishi wa habari,tunapofanya kazi zetu za uandishi wa habari tuzingatie weledi licha ya kuwepo kwa teknolojia mwandishi wa habari anafundishwa kufanya kazi katika misingi yake ya kiweledi ambapo uandishi wa habari una dhima kuu tatu ikiwemo kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha,”amesema Soko.
Pia ameziomba taasisi zote za kiserikali na binafsi waweze kufanya kazi na waandishi wa habari na kuhakikisha wanapata taarifa kwani lengo la waandishi ni kusaidia serikali ili kuibua vitu ambavyo siyo sahihi ambazo zinasaidia viongozi kuchukua hatua.
Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, katika maadhimisho hayo amesema wananchi wanahitaji kupata habari ambazo ni kamili.
Kalli amesema,habari ina nafasi kubwa sana katika taifa,ndio maana waandishi wa habari wanakila sababu ya kuhakikisha wanachuja habari zao na wanazo zipeleka ni sahihi hivyo wakumbuke wapo kwenye dunia ya ushindani.
“Mna kila sababu nyinyi wanahabari,muhakikishe habari zenu mnazokwenda kuzichukua ama kuzipeleka basi mkae chini mzichuje na ukipeleka jamii inasema barabara,tuzichuje na tufikirie ni habari muhimu katika taifa letu kujenga pamoja tukiwa wazalendo,”amesema Kalli.
Kwa upande wake Mratibu wa Programu wa taasisi ya Internews Tanzania Shaban Maganga, amesema kama taasisi wamekuwa wanatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na vyombo vya habari,ili waweze kuboresha maudhui na taarifa wanazozitoa.
“Kila Mei 3 ndio uwa tunaadhinisha siku ya uhuru wa habari,lakini mwezi mzima tunasema ni mwezi wa uhuru wa vyombo vya habari,katika muendelezo wa yale yanayoendelea katika mwezi huu Internews na MPC tukaona ni vyema sana waweze kuungana Mwanza ili waandishi wa habari, waweze kujadili yanayowahusu,”amesema Maganga.
Amesema kupitia mikutano kama hiyo itaweza kusaidia waandishi kutoa maoni na mawazo mbalimbali ambayo wanaamini kwa namna moja au nyingine utachangia kuboresha utendaji kazi wa waandishi wa habari pamoja na mazingira ya habari kwa ujumla nchini hapa.
Maganga amesema,hivi sasa serikali ya Tanzania ipo katika mchakato wa kufanya mabadiliko ya sheria ya habari na kwenye kongamano la juzi walisikia kwamba kufikia Septemba sheria zitakuwa zimeisha fanyiwa marekebisho hivyo ni dhamira nzuri.
Naye mmoja wa washiriki wa maadhimisho hayo Glory Kiwia, amesema kupitia maadhimisho hayo wameweza kujifunza vitu vingi ikiwemo kutumia mitandao ya kijamii kuhabarisha umma habari zilizo na ukweli na uhakika na namna ya kujilinda katika matumizi ya kimtandao.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi