December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WHO yatoa muongozo kubaini ukosefu madini chuma mwilini

Na Mwandishi Wetu, GENEVA

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo mpya wa kuweza kusaidia kubaini mapema ukosefu wa madini ya chuma mwilini sambamba na uwepo wa madini mengi ya aina hiyo kupita kiasi mwilini.

WHO inasema, mwongozo huo wa kipimo cha kiwango cha kemikali aina ya Ferritin ili kutathmni hali ya madini ya chuma mwilini, utasaidia wahudumu wa afya kutambua mapema ukosefu wa madini ya chuma na hivyo kuepusha madhara makubwa zaidi.

Ferritin ni aina ya protini inayopatikana kwa kiasi kidogo katika damu ya binadamu ambapo iwapo mtu akipimwa akiwa na kiwango cha chini ina maana kiwango cha madini ya chuma ni kidogo na iwapo protini hiyo ipo kwa kiwango cha juu, basi madini ya chuma nayo yapo kwa kiwango cha juu kupita kiasi.

WHO inasema kuwa, kiwango kidogo cha madini ya chuma kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili kinaweza kuwa na madhara yasiyotibika kwenye maendeleo ya ubongo wao na hatimaye kukwamisha uwezo wao wa kujifunza shuleni.

Kwa watu wazima, ukosefu wa madini ya chuma unasababisha uchovu, ukosefu wa tija kazini na hata ukosefu wa damu mwilini.

WHO inasema kuwa kwa upande wa kuwepo kwa kiwango cha juu cha madini ya chuma mwilini, nalo ni tatizo linaloweza kusababishwa na kurithi ambapo kutoa damu mara kwa mara ili kupunguza kiwango cha madini hayo mwilini kinaweza pia kuzorotesha afya ya mhusika iwapo hatopatiwa tiba.

Pia WHO inakumbusha kuwa, madini ya chuma ni muhimu sana mwilini hasa katika kusafirisha hewa ya oksijeni, uchambuzi wa vijinasaba na kuwezesha misuli kufanya kazi.

Akizungumzia mwongozo huo, Dkt.Francesco Branca ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula, WHO alisema kuwa, kuimarisha uwezo wa kutambua kiwango cha ukosefu wa madini ya chuma na hatari ya madini hayo kuwepo kwa kiwango kikubwa mwilini kutasaidia nchi kuamua mipango ya afya.

Ni kwa lengo la kufuatilia na kulinda wananchi wake hususani ukosefu wa madini ya chuma utokanao na lishe duni na miongoni mwa watu wenye maambukizi ya magonjwa.

UNICEF

Katika hatua nyingine, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetahadhariha kuhusu uwezekano wa mamilioni ya watoto katika eneo la Asia Magharibi kusumbuliwa na umaskini kutokana na janga la kiuchumi litakalosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Shirika la UNICEF limetangaza kuwa, katika mwaka huu watoto karibu milioni nane katika eneo la Magharibi mwa Asia wataathirika kutokana na kupotea kwa ajira milioni moja na laki saba kulikosababishwa na kufungwa mashirika, kutolipwa mishahara ya wafanyakazi na madhara mengine ya vizuizi vya karantini kwa umma.

Kwa mujibu wa Ted Chaiban ambaye ni Mkurugenzi wa UNICEF katika Kanda ya Asia Magharibi na Kaskazini mwa Afrika, kwa sasa karibu watoto milioni 110 wamesalia nyumba katika maeneo hayo na hawaendi shule kutokana na mlipuko wa maambukizi ya corona.

Aidha,tathmini ya UNICEF inaonyesha kuwa, watoto milioni 25 wamekuwa maskini na wakimbizi kutokana na mapigano huko Syria, Yemen, Sudan, katika ardhi za Palestina, Iraq na Libya.

Shirika hilo la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, linahitaji kiasi cha dola milioni 92 ili kuimarisha mapambano yake dhidi ya changamoto mbaya za virusi vya Covid-19.

Hata hivyo, hadi sasa watu 2,529,094 wameambukizwa virusi vya corona duniani na zaidi ya 174,573 wameaga dunia kwa maambukizi hayo.