June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WHI yaeleza Tanzania inauhaba wa nyumba milioni 3

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

 MKURUGENZI Mtendaji wa taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI), Dkt.Fred Msemwa amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa taasisi hiyo bado Tanzania   inakabiliwa na uhaba wa nyumba zipatazo milioni tatu huku ikiwa idadi ya  watanzania ikiwa ni zaidi ya milioni sitini.

 Ameeleza kuwa kwa jiji la Dar es salaam kuna uhaba wa nyumba laki nne pamoja na taasisi hiyo kujenga nyumba zaidi ya 100 katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Dkt.Msemwa ameelezwa hayo jijini hapa leo, Februari 9,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maendeleo ya Taasisi hiyo ambapo amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa upungufu wa nyumba imeelezwa kuwa ni asilimia 15 tu ya watanzania ambao wanaweza kumiliki nyumba ambazo thamani yake ni kuanzia shilingi milioni 25 hadi 30 na kuendelea.

“Hadi sasa WHI imejenga jumla ya nyumba 983 katika mikoa 19 ya Tanzania bara huku nyumba za gharama nafuu zikiendelea kujengwa katika mikoa yenye uhaba wa nyumba za walimu,watumishi na kada mbalimbali wenye kipato cha chini ili kupunguza uhaba wa nyumba,”amesema Dkt.Msemwa.

Aidha Dkt.Msemwa ameeleza kuwa bado watanzania hawajaweza kuwa na utayari wa kuwekeza katika sekta ya pesa kwa maana kuwa hawawezi kununua hisa na amana na kupelekea kuwa ni watanzania laki 8 pekee wenye kushiriki katika kuwekeza katika biashara ya fedha.

Amesema kuwa ili kuweza kuwa na nyumba bora na za bei nafuu taasisi imeona ni vyema pia watanzania wakawa na elimu ya umuhimu wa uwekezaji katika sekata ya pesa.

“Watanzania lazima wajue kuwa kuna tofauti sana ya kuwa na fedha na kuwekeza katika katika sekta ya kifedha kwani kuwekeza katika fedha na kuwa na nyumba bora na yenye gharama nafuu ni mambo ambayo yanafanana”ameeleza Dkt.Msemwa.

Pamoja na hayo Dkt. Msemwa amesema kuwa WHI imevuka lengo  kwa kukusanya michango za ya Sh. 12.95 huku matarajio yakiwa ni kukusanya Sh.bilioni 7.8 ikiwa ni ndani ya miezi miwili tangu kuanzishwa kwake kupitia mfuko wa Faida Fund.

“Makusanyo haya ya mfuko wa Faida Fund ni katika kipindi cha Novemba mwaka jana na mpaka kufikia Februari 9 tulikuwa na  Sh.bilioni 14, nabfedha hizo  tumeziwekeza katika masoko ya fedha ikiwemo mabenki na Serikali ambapo watanzania zaidi ya 4000 wamejiunga.

“Hapa nchini watanzania 80000 ndio wanaoshiriki katika uwekezaji wa pamoja wa soko la fedha, hivyo nawashauri watanzania kujitokeza kujiunga na mfuko huo ambao utawawezesha kufikia malengo, kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi,”amesema Msemwa.