October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa wilaya Tanga Thobias Mwilapwa akikagua ndoo za maji tiririka katika stendi ya mabasi yaendayo wilaya ya Pangani iliyopo eneo la Duga Mwembeni , Leo .(Picha na Hadija Bagasha, Tanga).

Wezi wa ndoo za maji kujikinga corona waibukia Tanga

Waiba ndoo za maji tiririka stend ya Daladala

Na Hadija Bagasha Tanga,

WAKATI mataifa mbalimballi duniani kote yakiendelea kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona, baadhi ya watu wasiojulikana jijini Tanga wameiba ndoo na koki za maji zaidi ya 10 za maji tiririka katika stendi kuu ya Daladala ya Ngamiani iliyopo barabara ya 12.

Ndoo hizo ambazo zilitolewa hivi karibuni na Chama cha Wamiliki wa Daladala jiji la Tanga (TAREMIA) kwa ajili ya kuisaidia mapambano dhidi ya Covid-19 na kuwekwa katika vituo vyote vya stendi za Daladala ili kusaidia abiria wanaokwenda maeneo mbalimbali.

Wakizungumza leo wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa katika stendi za Daladala zilizopo jijini Tanga, walibaini uwepo was wizi huo huku Wananchi wakisema, wezi hao walianza kuiba koki za kufungulia maji kwenye madumu na ndoo na baadaye walianza kuiba ndoo zenyewe nakufanya stendi hiyo kukosa kabisa vitakasa mikono hali inayofanya abiria na watumiaji wa stendi kuwa katika mazingira hatarishi.

Msimamizi wa Daladala katika stendi hiyo, Ally Kibaya amesema, wananchi wamekosa maji titirika baada ya koki na ndoo zote kuibiwa na watu wasiowatakia mema wananchi wenzao.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa ambaye alifika kituoni hapo kwa lengo la kukagua Daladala ikiwa zinatimiza maagizo ya Serikali yakutumia vitakasa mikono, amewatahadharisha waliofanya uhalifu huo na kusema ni hujuma inayochelewesha mafanikio ya wananchi juu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa Corona na kwamba yeyote atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Amesema wamepata Mapipa 10 makubwa yenye uwezo wa kubeba zaidi ya lita 2000 hadi 5000 za maji na mapipa hayo yatawekwa kwenye maeneo yenye mzunguko mkubwa wa wawatu ikiwemo maeneo ya stendi.