Na Lubango Mleka, Times Majira Online – Igunga.
WENYEVITI wa Serikali za mitaa Mamlaka ya mji mdogo Igunga mkoani Tabora wameilalamikia Halmashauri ya wilaya ya Igunga kwa kutowalipa posho zao za kila mwezi shilingi laki moja kwa zaidi ya miaka miwili na nusu.
Wenyeviti hao wametoa malalamiko hayo kwenye ofisi ya Mamlaka ya Mji mdogo Igunga wakati wakizungumza na waandishi wa habari na ueleza kuwa walishatoa malalamiko hayo kwa aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI Sulemani Jafo wakati huo, ambapo kwa sasa wamemuomba Waziri mwenye dhamana kuingilia kati suala hilo.
Wamesema hali hiyo imesababisha hadi wengine wameshastaafu na wengine kufariki jambo ambalo linawasababisha kuishi kwa shida pia walio kazini kuwa katika hatari ya kushawishika kupokea rushwa pindi wanapotoa huduma kwa wananchi.
Hawa Hamis mwenyekiti (viti maalumu) amesema wamekuwa wakifuatilia madai yao ya fedha mara kwa mara bila mafanikio.
“Kwa kweli sisi Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Mamlaka ya Mji Mdogo Igunga halmashauri yetu haitutendei haki kwani hizo posho za shilingi laki moja kila mwezi ni haki yetu lakini kila tunapofuatilia tumekuwa tukiahidiwa bila mafanikio,”.
Wamesema kuwa, kutokana na hali hiyo wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kwani wao ndio wana watu katika mitaa yao ambapo kila siku lazima watoe huduma mbalimbali na huduma zingine zinahitaji kuchapisha karatasi za vibali vya kuwapatia wananchi ikiwemo kupeleka mifugo yao mnadani, kudhamini Polisi na Mahakamani.
Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti miaka ya nyuma Amos Jegu amesema wakati huo walikuwa wakilipwa fedha hizo lakini ghafla zoezi hilo lilisitishwa bila sababu yoyote hadi anamaliza muda wake walikuwa wakiidai halmashauri milioni 11.1 ambapo hadi sasa hawajalipwa.
Naye Mwenyekiti wa sasa wa Mamlaka ya Mji Mdogo Igunga Fidel Mayunga amesema hadi sasa wanaidai Halmashauri ya Wilaya ya Igunga milioni 68.82 ambapo wamekuwa wakifuatilia bila mafanikio, jambo ambalo linawafanya waishi katika maisha magumu.
Akijibu malalamiko hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Benjamin Siperito amethibitisha kuwa wenyeviti hao ni kweli wanadai kiasi hicho cha fedha.
“Ni kweli malalamiko ya wenyeviti hao yako sahihi na sisi kama halmashauri tutaendelea kulipa fedha hizo kutokana na makusanyo ya fedha tutakayokuwa tukiyapata kupitia vyanzo vyetu vya mapato ya ndani,”amesema.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi