March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wenye viwanda waagizwa kuimarisha afya, usalama wa wafanyakazi

 Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewataka wamiliki wa viwanda na maeneo mengine ya kazi nchini,kuzingatia kanuni bora za usalama na afya ili kulinda nguvu kazi inayotumika katika uzalishaji viwandani.

Sangu ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kufuatilia umadhubuti ya mifumo ya usalama na afya katika kiwanda cha kusindika samaki cha Omega Fish Limited cha jijini Mwanza, ukiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi za kutembelea taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya kazi,ajira na mahusiano.

Amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha nguvu ya nchi inayotumika kutimiza malengo yake hususani utekelezaji wa Dira ya Taifa mwaka 2050 inalindwa kikamilifu,hivyo ameuelekeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pakazi(OSHA) kuwa karibu na kushirikiana na wawekezaji katika kusimika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pakazi.

“Kanda ya Ziwa inashughuli nyingi za kiuchumi ukiachilia mbali sekta hii ya uvuvi,kuna sekta nyingi kama vile ya madini ambapo kuna baadhi ya migodi bubu inayoanzishwa pasipo kufuata taratibu za isalama na afya,”amesema Sangu na kuongeza;

“OSHA fanyeni ukaguzi wa kina kwenye maeneo ya kazi nchini yakiwemo ya sekta ya madini,ili kuhakikisha kunakuwa na uzingatiaji wa taratibu zote muhimu za usalama na afya jambo ambapo ni muhimu katika kulinda afya za watu na kuongeza tija katika uzalishaji,”.

Awali Katibu wa jumuiya ya Viwanda vya Kusindika samaki Onesmo Sule,amesema changamoto zinazowakabili wasindikaji wa samaki nchini ni pamoja na upungufu wa malighafi unaosababishwa kwa kiwango kikubwa na shughuli za uvuvi haramu na kusababisha viwanda kuzalisha chini ya uwezo hivyo kuathiri ajira za watanzania na kupoteza mapato ya fedha za kigeni.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda,amesema ziara hiyo ya Waziri imelenga kufuatilia utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama na afya mahali pakazi katika kiwanda hicho kwa mujibu wa miongozo ya taasisi hiyo.