Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbarali
ASILIMIA kubwa ya wagonjwa wa macho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wanasumbuliwa na mtoto wa jicho kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wengi wao kuwa na umri mkubwa na wengine kutotambua dalili za mapema ili kutibu ugonjwa huo.
Daktari wa Macho katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni ya upimaji macho bure iliyofadhiliwa na taasisi ya Bilal Muslim, Dkt. Rehema Bidaga ameuambia Mtandao huu kuwa, tatizo la mtoto wa jicho linasumbua sana watu waliofikisha umri wa kuanzia miaka 60 na katika kampeni hiyo mbali na kutoa huduma za upimaji wa macho lakini pia walitoa huduma za upasuaji.
Amesema, jumla ya wagonjwa 50 walipatiwa huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho bila gharama yeyote kwa ufadhili wa taasisi ya Bilal Muslim kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya.
“Moja ya sababu inayosababisha wazee wengi kupata saratani ya mtoto wa jicho ni kuwa na magonjwa nyemelezi pamoja na yasiyoambukiza lakini pia kutozitambua dalili za awali kuhusu ugonjwa huo, ndio maana katika kampeni hii tukimpima tu akigundulika anaenda kufanyiwa upasuaji siku hiyo hiyo ,” amesema Dkt. Bidaga.
Zoezi hilo limekuwa na muitikio mkubwa sana kwa sababu wananchi kutoka kila maeneo ya wilaya walifika hospitalini hapo kufanya uchunguzi wa macho na kwamba maombi yao ni kuomba zoezi hilo liwe endelevu kwa sababu limeokoa gharama za matibabu.
Amesema kuwa, sababu nyingine inayosababisha wazee wengi kupata saratani ya mtoto wa jicho ni kushindwa kumudu gharama za matibabu ambapo wengi wao kutokana na hali za maisha wanashindwa.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma hiyo akiwemo Mwanyanje Deo ambaye ni mkazi wa Ilemi iliyoko Halmashauri ya Jiji la Mbeya amesema, taarifa za kutolewa kwa huduma hiyo ya macho alizipata kwa jamaa zake na kutokana na tatizo la macho ambalo limemsumbua kwa miaka mitatu sasa alilazimika kufunga safari hadi Mbarali kwenda kupata huduma hiyo.
Amesema alizunguka katika hospitaii mbalimbali kupata matibabu lakini hakufanikiwa kutokana na gharama kuwa kubwa na alipofika katika hospitali ya Mbarali alipata vipimo vyote bila gharama yeyote hadi upasuaji.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuendelea kutoa huduma bure za matibabu ya macho kwa wazee na makundi mengine kwa madai kuwa matatizo ya macho yanachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha nguvu kazi na uzalishaji kwa wategemezi wa familia.
More Stories
RPC Mbeya:Jeshi la Polisi tupo timamu kuhakikisha wananchi wanasherekea mwaka mpya kwa amani
NMB yadhamini kombe la Mapinduzi 2025
Songwe kuanza zoezi la kujiandikisha na kuboresha taarifa