Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Mbeya
WATU wenye ulemavu zaidi ya 100 wamepatiwa mafunzo ya elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili ,afya ya uzazi pamoja na ujasiriamali ili kuwawezesha kufahamu tabia zinazofanya mtu kuwa na afya nzuri na kuwakinga na maradhi mbalimbali.
Mafunzo hayo yametolewa na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya lengo likiwa ni kuwawezesha watu wenye ulemavu kuwa na utambuzi wa magonjwa hayo kutokana na mazingira walinayo na hata umuhimu katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ,Dkt.Godlove Mbwanji, akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo hayo, ameeleza kuwa, kundi la watu wenye ulemavu mara nyingi limekua ni rahisi kusahaulika.
Hivyo kama hospitali imeandaa mafunzo hayo ili kuawezesha kujiamini na kuona wao ni sehemu ya jamii katika kufanya mambo makubwa ikiwa ni jitihada za Serikali katika kutoa usaidizi wa kila namna kuhakikisha ustawi wa kila mmoja unazingatiwa.
“Hizi zote ni jitihada za serikali inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia katika kuthamini watu wenye ulemavu na kuhakikisha kwamba watu hawa nchi nzima wanathaminiwa, wapewa matibabu na elimu ili waweze kujikinga na magonjwa,”ameeleza DKt. Mbwanji.
Sanjari na hayo Dkt. Mbwanji ametoa wito kwa viongozi katika huduma za kijamii nchini kuendelea kuona namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu ili na wao waone ni sehemu muhimu ya jamii vilevile washiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Mkoa wa Mbeya Damasi Mwambeje,ameishukuru Serikali kwa kuwapatiwa mafunzo ya elimu ya afya na magonjwa mbalimbali.
Pamoja na somo la ujasiriliamali yaliyoratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwani kwa muda mrefu elimu hiyo haijawafikia wao kama watu wenye ulemavu kutokana na fikra potofu zilizoko kwenye jamii.
Ameeleza kuwa kundi hilo limekuwa likisahaulika katika masuala mbalimbali hivyo uongozi wa hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya imefanya jambo kubwa.
“Tunaomba taasisi zingine na wadau kuona umuhimu wa kuliona kundi hili kwa jicho la pekee ili kuokoa vizazi na vizazi vijavyo kwa maradhi mbalimbali ambayo kundi hili limeshindwa kuwa na utambuzi nayo,”ameeleza Mwambeje.
Katika mafunzo hayo zaidi ya washiriki 110 wenye ulemavu wamepataiwa mafunzo ya elimu ya magonjwa mbalimbali, Elimu ya Afya ya Akili, Ujasiriamali pamoja na kuchunguza afya bila malipo.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â