*Achukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti CHADEMA
*Ahaidi kushirikiana na Mwenyekti yoyote atakayeshinda
*Atamani chama kijiendeshe kwa mapato yake
Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Kanda ya Victoria,Ezekia Wenje,ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa(Tanzania Bara) wa chama hicho na wakati huo huo amechukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Wenje amechukua na kurejesha fomu hiyo Januari 3,2024,katika ofisi ya Kanda ya chama hicho zilizopo Nyegezi jijini Mwanza,mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari mkoani hapa,ambapo ameeleza nia ya kuwania nafasi hiyo ni kuwa amejipima na ameona anaweza,huku akieleza kuwa yupo tayari kushirikiana na Mwenyekiti atakayeshinda kuhakikisha chama hicho kinasonga mbele.
Ambapo amesema,uongozi unahitaji hekima busara,uvumilivu pamoja na kuwa msikilizaji huku akiwasihi wanachama wa chama hicho,kuwanadi wagombea bila kumtukana wala kumchafua mtu kwa kuweka akiba ya maneno kwani chama hicho ni kikubwa kuliko mtu yoyote.
“Kama unaniunga mkono,usimtukane mtu,niunge mkono kwa kujenga hoja,huwezi kunifanya mimi niwe msafi kwa kumchafua mwingine,kuna maisha baada ya uchaguzi.Nauvumilivu kamilifu,busara,hekima na subra ya kuwa Makamu Mwenyekiti Taifa wa CHADEMA,”amesema Wenje.
Pia Wenje amesema,mara baada ya kupata nafasi hiyo atashirikiana na kumshauri Mwenyekiti atakayeshinda kuboresha maeneo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha wanachama wa chama wanalipa ada,ili kuongeza mapato ya ndani ambayo yatasaidia chama hicho kujiendesha.
Eneo jingine ni kuimarisha uwajibikaji ndani ya chama hicho na kwa viongozi, ikiwemo kuweka vigezo ambavyo vitatumika kupima uwajibikaji kwa viongozi angalau kwa kila baada ya miezi mine pamoja na mafunzo ya viongozi ndani ya chama.
Pamoja na kuboresha uhusiano wa ndani nan je ya nchi,ikiwemo wa viongozi wa dini,vyama vya siasa,asasi za kiraia na wananchi.Pia atasimamia maadili ya chama kwani kwa sasa kuna baadhi wa watu wanatumia mitandao ya kijamii ikiwemo kutengeneza magroup wa WhatsApp,na kuwaunga viongozi kisha kuwashambulia kwa matusi.
Sanjari na hayo amesema, atasimamia CHADEMA Digital, kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha ambayo yatatumika kuendeleza chama hicho pamoja na kuwalipa viongozi posho.
More Stories
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika
TANESCO yarudisha shukrani kwa jamii