Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Viongozi zaidi ya 60 wa taasisi za kiraia wamejitokeza kupata mafunzo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Kiislamu nchini Tanzania (TAMPRO) juu ya namna ya kuandaa andiko la mchanganuo wa mradi linaloweza kuvutia wafadhili kutoa fedha.
Mwenyekiti wa TAMPRO, Haji Mrisho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wingi huo wa washiriki waliojitokeza unaakisi uhitaji mkubwa wa ujuzi huo hasa miongoni mwa viongozi wa taasisi za Kiislamu. Mrisho alisema TAMPRO waliona uhitaji huo mapema na hivyo kuamua kuandaa mafunzo hayo ili kuzijengea uwezo taasisi hizo za kiraia.
Kwa mujibu wa Mrisho, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango-mkakati wa miaka minne na mpango kazi wa mwaka mmoja wa taasisi hiyo. Pia aliahidi kuwa huu ni mwanzo tu wa mfululizo wa mafunzo mengi yatakayoandaliwa na TAMPRO ili kusaidia taasisi hizo kukabiliana na ukosefu wa fedha na changamoto nyingine tofauti.
“TAMPRO, ikiwa jumuiya yenye wasomi, wenye taaluma mbalimbali, tunao wajibu wa kusaidia taasisi za kiraia kukabiliana na changamoto hizi. Safari hii, tumeona tuwaite viongozi hawa wa taasisi za kiraia ili tuwaelekeze vyanzo mbalimbali vya kujipatia mapato, hususan wafadhili,” alisema Mrisho.
Mwenyekiti Mrisho, ambaye binafsi yake ana uzoefu mkubwa katika masuala ya uandishi na usimamizi wa miradi katika taasisi za kiraia, alisema kilichosisitizwa kwenye mafunzo hayo ni mambo ambayo wafadhili wanaangalia kabla ya kutoa fedha ikiwemo thamani ya pesa yao wanayotoa ukilinganisha na huduma zinazoombewa pesa (value for money), uwazi wa mifumo na uwajibikaji wa kifedha.
Katika semina hiyo, moja ya changamoto zilizotajwa ni maandiko ya mchanganuo kutokidhi vigezo vya wafadhili na hivyo waombaji kutopewa fedha. Kutokana na changamoto hiyo, mkufunzi aliyeendesha mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdallah Katunzi, alianisha maeneo kadhaa ya udhaifu.
Akifafanua, Katunzi alisema wadhamini na wafadhili hutoa fedha kwa kuangalia vitu viwili vikubwa: thamani ya muombaji aliyoiita ‘credibility’ kwa kiingereza na uzuri wa andiko.
Kuhusu uzuri wa andiko, Katunzi alitumia muda mwingi kuelezea namna ya kuibua tatizo halisi, la kipekee na mahsusi na namna ya kulielezea tatizo hilo kiufasaha. Pia, mkufunzi huyo alielezea namna ya kutohoa malengo ya mradi kutokana na vyanzo vya tatizo.
Mwingine aliyepata fursa ya kuwasilisha mada alikuwa ni Mohammed Kamilagwa kutoka kampuni ya Silent Ocean ambaye alizungumzia namna taasisi za kiraia zinavyoweza kupata ufadhili kutoka sekta binafsi, akiwaibia siri washiriki hao kuhusu mitazamo ya makampuni binafsi.
Kamilagwa aliwatajia washiriki vigezo muhimu ambavyo kampuni binafsi zinaangalia kabla ya kuamua kufadhili mradi au shughuli kuwa ni pamoja na uwepo wa andiko la kitaalamu likijumuisha data/takwimu kuonesha athari ya jambo linaloombewa pesa. Kigezo kingine, alisema, ni namna kampuni husika itafaidika kutokana mradi huo.
“Vitu hivyo viwili, yaani uzuri wa andiko na namna tunavyofaidika, ni vigezo vya msingi ambavyo vinatuongoza sisi, kama kampuni binafsi, kuona jinsi gani tunasaidia ile jamii ikafaidika na kuisaidia serikali pale penye mapungufu wakati jamii inahitaji hiyo sapoti,” alisema Kamilagwa.
Licha ya mada zilizowasilishwa, washiriki walipata fursa ya kufanya mazoezi ya kuibua mawazo ya miradi, kuyaandikia maelezo ya tatizo na malengo. Pia, washiriki walipata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu, huku baadhi ya waalikwa kutoka taasisi za wafadhili wakitoa msaada wa ufafanuzi katika mambo mbalimbali.
TAMPRO ni taasisi iliyoanzishwa mwaka 1997 kwa ajili ya kuwaleta pamoja wanataaluma wa Kiislamu ili watumie ujuzi wao katika kusaidia Watanzania kuboresha ustawi wao. Wanataaluma wote wa Kiislamu wanaweza kujiunga na taasisi hii. Kupitia kliniki (idara) zake sita, TAMPRO imekuwa ikiendesha miradi mbalimbali inayogusa moja kwa moja jamii katika sekta za elimu, afya, biashara, habari na Tehama na hata katika nyanja ya dini.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua