Mwandishi: Ismail Mayumba
Katika ulimwengu wa kidijitali wa sasa, barua pepe ni nyenzo muhimu sana kwa mawasiliano ya kikazi na taasisi. Miongoni mwa chaguo zinazotumika sana ni Webmail na Business Gmail (Google Workspace).
Webmail ni huduma ya barua pepe inayotolewa na kampuni za hosting (uhifadhi wa tovuti) na hutumika kupitia kivinjari cha mtandao (browser) kama Chrome au Firefox kwa anuani kama mail.domain.com, mara nyingi ikitumia mifumo kama Roundcube au Horde.Â
Business Gmail, kwa upande mwingine, ni huduma ya barua pepe ya kitaalamu inayotolewa na Google ambapo mtumiaji hupata barua pepe yenye jina la domain ya kampuni yake, kwa mfano info@kampuni.co.tz, lakini kwa kutumia mfumo kamili wa Gmail unaofahamika na wengi.
Watu wengi hudhani Business Gmail ni ile Gmail ya kawaida inayomalizika na @gmail.com, jambo ambalo si sahihi, kwani Business Gmail ni huduma maalum inayoruhusu taasisi kutumia domain zao huku zikifaidika na mazingira ya Gmail. Ingawa kwa miaka mingi taasisi na ofisi nyingi zimezoea kutumia webmail, teknolojia hizi mbili zinafanana na kutofautiana katika maeneo muhimu yanayoathiri ufanisi na usalama wa mawasiliano ya kikazi.
Katika integration (muunganiko) na software (programu) zingine, zote zina uwezo wa kuunganishwa na mifumo mingine kupitia mbinu za msingi kama SMTP, IMAP, na POP3 (itifaki za mawasiliano ya barua pepe), lakini Business Gmail huongeza urahisi zaidi kwa kuunga mkono API (miunganisho ya programu), OAuth (uthibitishaji salama), na integrations za moja kwa moja na mifumo ya kisasa ya biashara na elimu, huku webmail ikifaa zaidi kwa mazingira rahisi yanayohitaji muunganiko wa kawaida.
Kwa upande wa file sharing (ushirikishaji wa mafaili), huduma zote mbili huruhusu kutuma na kupokea mafaili kupitia barua pepe, ambapo webmail hufanya hivyo kwa kuambatanisha mafaili moja kwa moja, jambo linalotosha kwa nyaraka ndogo na matumizi ya kawaida, ilhali Business. Gmail huongeza uwezekano wa kushirikisha mafaili kupitia mfumo wa uhifadhi uliounganishwa, unaoruhusu kudhibiti ruhusa kama kusoma au kuhariri.
Kuhusu storage (uhifadhi wa data), webmail hutoa nafasi ya kuhifadhi barua pepe kulingana na kifurushi cha hosting kilichochaguliwa, ambacho kinatosha kwa matumizi ya kawaida, wakati Business Gmail hutoa storage inayounganishwa na huduma nyingine za akaunti hiyo, hivyo kuwezesha mtumiaji kupanga na kuhifadhi taarifa kwa mtiririko mmoja.
Katika availability (upatikanaji wa huduma), zote mbili zimeundwa kupatikana mtandaoni muda wote mradi kuna intaneti, ambapo webmail hutegemea zaidi uimara wa server za hosting na Business Gmail hutumia miundombinu ya wingu (cloud infrastructure) ili kuhakikisha huduma inapatikana kwa watumiaji katika maeneo mbalimbali.Â
Kuhusu pricing (gharama), webmail mara nyingi huja kama sehemu ya kifurushi cha hosting kwa gharama nafuu, ilhali Business Gmail hulipiwa kwa mtumiaji kulingana na mpango uliochaguliwa, huku kila moja ikitoa thamani kulingana na bajeti na mahitaji ya taasisi.Â
Katika eneo la cyber security (usalama wa mtandao), zote zinazingatia ulinzi wa barua pepe kwa kutumia SSL/TLS (usalama wa mawasiliano), uthibitishaji wa nenosiri, na ulinzi dhidi ya spam, huku Business Gmail ikiongeza hatua za ziada kama uthibitishaji wa vipengele viwili (two-factor authentication) na ufuatiliaji wa shughuli zisizo za kawaida.
Kwa ujumla, webmail ni chaguo linalofaa kwa kampuni ndogo na za kati zinazohitaji suluhisho rahisi na la gharama nafuu, ilhali Business Gmail inafaa zaidi kwa makampuni makubwa, taasisi, au mashirika yenye matawi mengi ndani na nje ya Tanzania yanayohitaji ufanisi wa juu, muunganiko mpana wa mifumo, na kiwango cha juu cha usalama wa barua pepe zao.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria