Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeikabidhi Jumuiya ya Maendeleo kwa Wasioona Tanzania (Tanzania Association of the Blind -TAB) machapisho ya nukta nundu pamoja na fimbo nyeupe ikiwa ni jitihada za kuunga mkono maendeleo ya watu wenye mahitaji maalum.
Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya maandishi ya nukta nundu (Braille Day) ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda.
Wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi – WCF, Dkt. John Mduma amesema, katika kutekeleza majukumu yake, WCF imeendelea kushirikiana na Makundi Maalum wakiwemo watu wasioona kwenye masuala mtambuka ikiwemo Elimu.
“Tunatambua kuwa kundi hili linakabiliana na changamoto ya kupata taarifa kwani machapisho mengi hutolewa katika maandishi ya kawaida, WCF imechapisha miongozo inayotoa elimu ya fidia kwa wafanyakazi kwa nukta nundu (braille) kwa ajili ya wale ambao hawawezi kusoma maandishi ya kawaida”,.
“Mfuko unatambua wanachama wasioona ni miongoni mwa wadau muhimu sana chini ya Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu ambao wapo katika kada mbalimbali nchi nzima na miongoni mwao ni waajiriwa wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi hivyo ni imani yetu kuwa miongozo hii itawaongezea uelewa kuhusu haki za msingi ikiwemo fidia kwa wafanyakazi na watakuwa mabalozi wazuri wa WCF”, amesema Dkt. Mduma.
Zaidi ya machapisho hayo, WCF imekabidhi pia fimbo nyeupe ili kuwarahisishia kundi hilo utekelezaji wa majukumu ya kila siku katika kujenga uchumi wa Taifa letu.
“WCF itaendelea kushirikiana na wadau hawa muhimu ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuleta maendeleo kwa makundi yote”, amesema Dkt. Mduma.
Akitoa salamu za Serikali kufuatia msaada huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameipongeza WCF kwa kushirikiana na kundi hili maalum kwani hatua hiyo inaendana na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka Taasisi za Umma kuboresha huduma na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa, Serikali ipo katika hatua za mwisho za uchapaji vitabu vya maandishi ya nukta nundu kwa shule za sekondari pamoja na wanafuzi wasioona kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kwa masomo ya sanaa, sayansi na biashara na elimu ya awali.
“Kwa mwaka 2020/21, Serikali imechapa na kusambaza vitabu vya maandishi yaliyokuzwa na ya Braille kwa wanafunzi wasioona kuanzia darasa la kwanza hadi la saba pamoja na kuchapa vitabu vya kidato cha tano hadi cha sita ili kuhakikisha wanafunzi wasioona wanakuwa na vitabu vya kiada sambamba na wanafunzi wengine”, amesema Profesa. Mkenda.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best