November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Ujenzi kufanya ziara ya kushtukiza

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho amesema atafanya ukaguzi wa kushtukiza katika taasisi zilizo chini ya Wizara yake, lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi katika taasisi hizo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyanyakazi wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi), Waziri huyo amesema ukaguzi huo utaenda sambamba na kufanya mabadiliko ya uongozi na wafanyakazi wa taasisi hizo, endapo utendaji wao utakuwa hauridhishi.

“Kuna taasisi ambazo zimekuwa na malalamiko ya hapa na pale, kwa sababu Wizara ni sikivu tumeyasikia na tutapita kufanya ukaguzi katika taasisi hizi, endapo tutakuta watendaji wa taasisi hizi wanafanya ndivyo sivyo, hatutasita kufanya mabadiliko stahiki ili tuendane na matarajio ya Watanzania wote,” amesema.

Amewataka watumishi wa sekta hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, juhudi, maarifa, maadili ya fani husika na maadili ya utumishi wa umma ili kuleta utendaji wenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Dkt. Chamuriho ametoa wito kwa Menejimenti ya Wizara na taasisi zote za Wizara, kuhakikisha thamani ya fedha na ubora katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miradi ya ujenzi inaonekana wazi wazi na kuzingatiwa kwa mujibu wa vigezo na viwango vilivyowekwa.

Amesema serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha ukaguzi wa ubora wa barabara na viwanja vya ndege, ikiwa ni pamoja na kutumia mitambo maalumu ya ukaguzi ili kuokoa matumizi ya fedha nyingi za serikali na kuongeza ubora wa miradi yote ya ujenzi nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa sekta hiyo, Mhandisi Joseph Malongo amesema kuwa Kikao hicho kitajadili masuala mbalimbali ya watumishi kwa nia ya kutimiza lengo la kuboresha ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi mahali pa kazi.

Ameongeza kuwa, Wizara kupitia sekta hiyo inaendelea na jitihada za kudhibiti ubora wa usimamizi wa ujenzi wa miradi ya barabara, majengo, madaraja, vivuko, huduma za ufundi na umeme pamoja na viwanja vya ndege lengo ni kuhakikisha viwango vya ujenzi vinafikiwa na pia kupunguza gharama za miradi.

Naye Katibu wa Baraza hilo, Wakili Fanuel Muhoza akizungumza kwa niaba ya watumishi wa sekta hiyo amesema, wataendelea kufanya kazi kwa kushirikiana, uadilifu pamoja na weledi ili kuhakikisha sekta hiyo inafikia malengo yake iliyojiwekea.

Mkutano huu wenye ajenda ya kujadili Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22, umeshirikisha wajumbe mbalimbali kutoka wizarani na taasisi mbalimbali za sekta hiyo.