Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japan, Konosuke Kokuba anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini mnamo mwezi Januari mwaka 2024.
Katika ziara hiyo, Kokuba ataongozana na ujumbe wa watu 40 kutoka kampuni binafsi zinazojihusisha na masuala ya miundombinu na baadhi ya watumishi wa Wizara yake.
Ziara hiyo imelenga kujadili fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika maendeleo ya miundombinu.
Hayo yamejulikana (07/12/2023) katika kikao cha pamoja cha maandalizi ya ziara hiyo kilichoshirikisha viongozi wa Wizara ya Uchukuzi na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bwana Plasduce Mbossa pamoja na Menejimenti yake kilichofanyika jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara.
Kwa upande wa Japan, ujumbe wake umeongozwa na Bwana Yoshihiro Kakishita kutoka Sekretarieti ya Wizara ya Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii ya Japan.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbosaa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Japan kuja kuwekeza kwa upande wa miundombinu ya Bandari nchini.



More Stories
Mradi wa kuimarisha huduma za dharura kwa majeruhi wa ajali za barabarani wazinduliwa
MSIGWA:Mfumo wa usajili waandishi wa habari kidijitali upo mbioni kukamilika
Kongani ya Viwanda ya Sino _Tan kutoa ajira laki moja