November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Katiba na Sheria ataka mradi ukamilike kwa wakati

Judith Ferdinand na Daud Magesa,TimesMajira Online, Mwanza

Mkandarasi wa mradi wa Kituo Jumuishi cha Taasisi za Kisheria za Serikali Mkoa wa Mwanza,SUMA JKT ametakiwa kukamilisha mradi huo ifikapo Oktoba 23, mwaka huu,ili wananchi waanze kupata huduma.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria,Dkt. Damas Ndumbaro,wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala Bora,Katiba na Sheria,ambapo ameeleza kuwa mradi huo wa miezi 18 kwa mujibu wa mkataba unatakiwa ukamilike Oktoba 23, mwaka huu, hadi sasa umefikia asilimia 45 badala ya asilimia 55.

“Serikali haidaiwi na haijachelewesha malipo,tuliwapa kazi hiyo tukifahamu mna uwezo wa kufanya kazi saa 24 hatutegemei ucheleweshaji wowote na hatutaongeza, hakikisheni mnakamilisha ifikapo Oktoba 23, mwa huu wananchi waanze kupata huduma,”ameeleza.

Waziri huyo wa Sheria na Katiba aliongeza kuwa hategemei gharama kuongezeka sababu ya kuchelewa kwa mradi,hivyo waendelee kushirikiana ili wananchi wanufaike.

Mbunge wa Kishapu,Boniface Butondo alionyesha wasiwasi huenda mkadarasi akashindwa kutekeleza mradi huo ndani ya miezi nane iliyobaki kwani walitegemea uwe umefikia asilimia 65 badala ya 45 sasa.

Mbunge wa Singida Kaskazini,Ramadhan Ighondo alimtaka mkandarasi aongeze kasi ya utendaji,nguvu kazi na muda afanye kazi usiku na mchana,asitegemee kuongezwa muda maana gharama zitaongezeka na anapopata changamoto ya malipo aiambie serikali pia ilipe kwa wakati mradi usikwame.

Aidha Mbunge wa Viti Maalum kundi la Walemavu,Khadija Kaaya ‘Keisha’ ameeleza kuwa matatizo ya miradi kuchelewa ni yale yale na yanajirudia, hivyo tutafute tiba ili tufaye kazi kwa ufasaha.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala Bora, Katiba na Sheria,Florent Kyombo, ameeleza kuwa licha ya ucheleweshaji kidogo wa mradi mambo yaliyochangia ama kurudisha nyuma utekelezaji yafanyiwe kazi ili kuendana na kasi inayotakiwa na kuukamilisha.

“Tumeubariki mradi huu na tunauhitaji sana ili kuwapunguzia wananchi gharama na umbali wa kufuata huduma,mradi ni mzuri hivyo ongezeni kasi kama tulivyokubaliana ukamilike kwa muda uliopangwa,”ameeleza.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Kapteni Ferdinand Sira, ameeleza kuwa mradi huo una changamoto mbalimbali zilizochangia uchelewe kwa miezi miwili ambapo wameandaa mpango kazi utakaoendana na muda wa kukamilika kwa mradi.

Aliahidi kufanya kazi usiku na mchana kutekeleza mradi huo kwa weledi na juhudi ili ukamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa na kuishukuru Kamati hiyo ya Bunge kuwatembelea kuona maendeleo ya mradi huo.