May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya kudumu ya Bunge ya utawala katiba na sheria yaridhishwa na hatua za ujenzi Ofisi ya msajili na kiwanda cha uchapaji nyaraka

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma.

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria imeonesha kuridhishwa na hatua ya ujenzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ujenzi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali Mjini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Joseph Mhagama,katika ziara ambayo ililenga kujionea kile ambacho kimepangwa kwenye bajeti ya Serikali na kuangalia hatua zilizopigwa, changamoto zilizojitokeza na namna ya utatuzi wake.

“Ziara hii imetuwezesha kupata uhalisia wa hali jinsi ilivyo, ili iweze kutusaidia wakati wa kupanga bajeti, tuwe na uhalisia wa utekelezaji miradi,”amesema.

Akizungumzia kuhusu Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Mhagama amesema upo muhimu wa Idara hiyo kuwa na mifumo rasmi ya kujisimamia bajeti yake yenyewe (kama wakala) ili isaidie idara hiyo iweze kuingia katika soko shindani.

Amesem kuwa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ikiweza kujisimamia katika bajeti yake, itasaidia kuongeza Makusanyo mengi ambayo yanategemewa kutoka katika Idara hiyo.

“Tunachangamoto kubwa sana katika utengenezaji wa nembo ya Taifa,lazima tuwe na Mamlaka moja ya kutengeneza nembo ya Taifa na watu wengine wote waipate kupitia katika Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali,”amesema Mhagama.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema anakubaliana na maelekezo ya Kamati.

Ambapo amesema kuwa Wizara itatoa taarifa mbele ya Kamati hatua iliyofikia katika kuandaa mabadiliko ya sheria ili kuwezesha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa wakala.

Naye Ahmed Ngwali Mjumbe wa Kamati, ameshauri Idara ya Mpiga Chapa Mkuu Wa serikali Kufanyia kazi mapendekezo ya Kamati mapema ili iweze kubadilishwa na kuwa wakala.

Awali Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali George Lugome amesema Utakapokamilika mradi wa Kiwanda cha Uchapaji wa Nyaraka za Serikali itasaidia kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu ikiwa ni sambamba na kuongeza ajira na kuwa sehemu ya mafunzo kwa watu wanasomea masuala ya uchapishaji.