December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali : Mgonjwa wa Marburg aliyepona aruhusiwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MGONJWA mmoja wa Marburg mwenye umri wa miaka (26) ameruhusiwa akiwa na afya njema na jamii imetakiwa kumpokea vyema na kushirikiana nae katika shughuli zake.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Marburg ulioripotiwa Wilaya ya Bukoba vijijini mkoani kagera.

“Ninayo furaha kubwa kuwajulisha kuwa leo tumemruhusu mgonjwa mmoja mwanaume mwenye umri wa miaka (26) akiwa na afya njema, ni matumaini yangu jamii itampokea vyema na kushirikiana nae kama kawaida, ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hatujapata wagonjwa wapya wala vifo”.

Aidha, tangu kuripotiwa ugonjwa huu Machi 21, 2023 kufikia Aprili 4, 2023 jumla ya visa ni 8 na vifo 5.Waziri Ummy ameongeza kuwa wagonjwa wawili waliolazwa wanaendelea vizuri na matibabu katika vituo maalumu vilivyoandaliwa.

Hata hivyo Waziri amesema kuwa jumla ya watu 212 waliotengamana na wagonjwa wamebainishwa na kati ya hao watu 35 wamemaliza siku 21 za uangalizi bila kuonesha dalili zozote za ugonjwa .

“Hii ni ishara nzuri sana kwetu, Wizara ya afya , serikali na taifa kwa ujumla kwa kuwa maambukizi ya Virus vya Marburg nchini yamedhibitiwa kwa wakati.Serikali bado inahimiza wananchi wote na hasa wa Mkoa wa kagera kuendelea kuchukua tahadhari, kudhibiti na kuzuia maamb ukizi mapya katika jamii”.

Vilevile Waziri Ummy amewahakikishia watanzania na jamii ya Kimataifa kuwa Tanzania ni salama hivyo wananchi waendelee na shughuli na safari bila hofu yeyote na kwamba serikali bado inahimiza wananchi wote hasa wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari kudhibiti ugonjwa na kuzuia maambukizi mapya katika jamii.