December 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WAZIRI UMMY:Bima ya Afya kwa wote haitakuwa na matabaka

Na Emmanuel Malegi-WAF,Dodoma

WAZIRI wa afya ,Ummy Mwalimu amesema Muswada wa bima ya afya unalenga kutoa huduma za matibabu kwa wananchi wote bila kujali tajiri au maskini hivyo hautakua na matabaka.

Waziri Ummy amesema hayo leo 18 Oktoba 2022 wakati akiwasilisha muswada huo mbele ya Kamati ya Kudumu ya kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema muswada huo bado haujapitishwa hivyo wizara inaendelea kupokea maoni kutoka katika makundi mbalimbali nchini ili kuweza kuiboresha na kuwa bima yenye manufaa kwa wananchi wote.

Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa huduma zitakazotolewa kwa mwananchi itategemea na michango yake aliyochanga katika kipindi fulani ili kuepuka kugharamia huduma zenye gharama kubwa kwa mgonjwa aliyechangia mwezi mmoja hivyo kupelekea mfuko kuteteleka na hatimaye kuanguka na kushindwa kutoa huduma, hivyo amewataka wananchi kujiunga na kuchangia mapema kabla ya kuugua.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo amesema kamati yake itakutana na wadau mbalimbali ili kupokea maoni yao kabla ya kutoa maoni ya jumla, lengo likiwa ni kuboresha muswada huo kabla haujapitishwa na kuwa sheria rasmi.

Nyongo amesema lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake ili wawe na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapougua hivyo muswada huo unatakiwa kupitiwa kwa uangalifu ili uguse wananchi wote bila kikwazo cha kiuchumi.