November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ummy: Ugonjwa wa Malaria umepungua nchini kwa silimia 7.5

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

WAZIRI wa afya Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa malaria umepungua Nchini Tanzania kutoka asilimia 14 mwaka 2012 hadi asilimia 7.5 mwaka 2017.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa afua ya unyunyiziaji dawa ya viuadudu vya kibaolojia kwenye mazalia ya mbu uliofanyika Mkoani Tanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo balozi wa Uswis Nchini Tanzania.

Waziri Ummy amesema kuwa ugonjwa wa malaria bado ni tatizo kubwa katika Nchi yetu kwani katika kila wagonjwa 100 wanaofika katika hospitali wagonjwa 10 wanafika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa changamoto ya ugonjwa wa malaria.

Waziri Ummy amesema kuwa pamoja na serikali kutekeleza afua ya kuua viluilui vya mbu kwa kutumia viuadudu wataendelea pia kutekeleza afua nyingine za kudhibiti ugonjwa malaria ikiwemo mazingira yanakuwa masafi wakati wote.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa kayika ajira mpya ambazo Rais atatoa kibali atahakikisha kata zote zinakuwa na maafisa afya nchini ili waweze kusimamia afua mbalimbali za afya.

“Hili swala ni la kufa na kupona kwetu sisi kama Wizara ya afya na mimi sio waziri wa wagonjwa ni waziri wa afya jukumu langu la kwanza ni watu wasiumwe hivyo ni lazima kama wizara tuweke nguvu katika kinga sababu kinga ni bora zaidi kuliko tiba mimi naona aibu watu wanapopelekwa hospitali kwajili ya kuharisha na kipindupindu sababu ya uchafu, “alisisitza Waziri Ummy.

Aliongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa Nchi inapoteza zaidi ya bilioni 400 kwa mwaka kwasababu ya uchafu sisi kama Wizara ya afya tunaamini tukiwekeza kwrnye kinga tutaweza kuokoa maisha ya watu na wagonjwa mbalimbali.

Hata hivyo Waziri Ummy amesema mtu yeyote ambaye hatatekeleza wajibu wake katika kuharibu mazalia ya mbu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria inavyotaka.

“Tunaamini kabisa hii ikifanyika kikamilifu itasaidia kupunguza idadi ya mazalia ya mbu, kupunguza wingi wa mbu katika maeneo tunayoishi na hatimaye kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine yanayoenezwa na mbu ikiwemo ugonjwa wa Dengue, homa ya manjano, matende, mabusha pamoja na Chikungunya, “alibainisha Waziri Ummy.

Aidha waziri Ummy ametoa wito kwa watendaji wa Halmashauri tatu za Mkoa wa Tanga zinazotekeleza afua hiyo kuipa umuhimu afua hiyo ili iweze kuwapunguzia mzigo wa kununua dawa.

Balozi wa Uswis Nchini Tanzania Didier Chassot amesema Uswis itaendelea kushirikiana na Tanzania kumaliza ugonjwa wa malaria ambao bado umeendelea kuwa tatizo katika nchi yetu.

Balozi huyo amesema kuwa pamoja na juhudi za serikali ya Tanzania na washirika wake ugonjwa malaria bado upo na bado unaendelea kusababisha vifo.

“Sisi kama wadau tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuhakikisha ugonjwa wa malaria unatokomezwa tuko hapa kwajili ya kupambana na afua ya umwagiliaji viuadudu kwenye mazalia ya mbu tutaendelea kushirikiana na wizara yako, “alisisitiza Balozi huyo.

Aidha alisema Uswis itaendelea kushikana mkono na Tanzania kutokomeza malaria hivyo ameitaka jamii yote kuchukua hatua ya kupambana na ugonjwa huo.

Mradi huo wa malaria unatekelezwa na serikali ya Uswis kwa kushirikiana na Tanzania na unafanywa katika wilaya tatu kwenye Mkoa wa Tanga ikiwemo wilaya ya Tanga, Handeni na Lushoto.