Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu ametishia kuwaondoa walimu wakuu wanaoendelea kuchukua michango ya fedha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kusababisha vikwazo vya kielimu kwa wazazi.
Pia waziri Ummy amewaelekeza wakurugenzi wa Halamashauri zote nchini kuhakikisha wanatumia mapato yao ya ndani kajenga matundu ya vyoo kwajili ya wanafunzi kupitia mradi wa madarasa mapya wanayojenga nchi nzima.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya 14 na ofisi mbili za walimu katika shule ya sekondari Saruji yaliyojengwa kwa fedha za Uviko 19.
Waziri Ummy amesema hatosita kuwachukulia hatua walimu wakuu watakaobainika wanaendelea kuchangisha michango isiyofuata utaratibu mashuleni jambo ambalo amelikemea vikali na kusema Rais Samia amesisitiza elimu iendelee kutolewa bure bila malipo yeyote.
Sambamba na hayo waziri Ummy ameagiza kufikishiwa taarifa ya mwalimu yeyote atakayebainika anaendesha michango bila utaratibu mashuleni jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya serikali.
“Katika hili sitanii tumeshashusha vyeo walimu wakuu wawili ndani ya wiki mbili tuleteeni taarifa ya shule yeyote ambayo ina michango isiyofuata utaratibu Rais Samia anaendeleza elimu bila malipo, Rais Magufuli alianzisha sera hii alikuwa anatoa bilioni 23 kila mwezi Rais Samia ameongeza bilioni 26 kutoka bilioni 23 lol mwezi kwajili ya kugharamia sekta ya elimu, “amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri Ummy amewataka wakuu wa wilaya kutosita kuwachukulia hatua mwalimu mkuu yeyote kwani tunataka tuondoe vikwazo visivyo vya lazima kwa watoto wa kitanzania katika kupata elimu.
Waziri Ummy amesema Rais amewawezesha kujenga madarasa ya sekondari elfu 12 na shule shikizi 3000 nchi nzima ambapo ameagiza kila darasa moja linapaswa kuwa na matundu mawili ya vyoo.
Aidha Waziri Ummy amesema lengo la serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanakwenda shule bila vikwazo vyovyote hususani kwa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza.
“Niwaelekeze wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kama walivyofanya Halmashauri ya jiji la Tanga kajenga matundu ya vyoo kwajili ya wanafunzi, “amesisitiza waziri Ummy.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amesema wamekamilisha kwa aslimia 100 ujenzi wa shule zote katika jiji la Tanga na kupendekeza shule hiyo badala ya kuwa ya mchanganyiko iwe ya wasichana watupu ili waendelee kutoa hamasa kwa wanatanga.
“Mheshimiwa Waziri kama itakupendeza shule hii tuiite jina lako na hii kuthamini na kutambua mchango wako mkubwa kwa wanatanga na watanzania kwa ujumla, “amesisitiza Mgandilwa.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya Maweni anayesimamia ujenzi wa shule hiyo Mpokigwe Anyatike amempongeza Rais Samia kwa kuwapatia fedha hizo ambazo zimeweza kutatua changamoto ya madarasa jijini Tanga.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari