January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndumbaro mgeni rasmi uzinduzi wa Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia Kigoma

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro Leo tarehe 23 Januari,2025 amewasili Mkoani Kigoma na kukutana na mwenyeji wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  Thobias Andengenye, kwa ajili ya kushiriki katika Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia utakaofanyika tarehe 24 Januari, 2025 Mkoani Kigoma.

Akizungumza mara baada ya Waziri  kuwasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya salamu, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema kuwa ameipongeza  Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila Mwananchi anapata Haki na kwa wakati kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro amesema kuwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria Migogoro mbalimbali itakwenda kutatuliwa kupitia njia ya Amani, Usuluhishi, Mahakama, Kiutawala na kwa njia za Kiuchunguzi.

Ndumbaro amesema kuwa,  Kampeni ya Msaada wa Kisheria itatekelezwa kwa muda wa siku tisa katika Halmashauri tisa za Mkoa wa Kigoma na kuwafikia Wananchi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha matatizo yote ya Kisheria yanapatiwa suluhu.