January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndalichako ampongeza Rais Samia kwa kufungua fursa za uwekezaji nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufungua fursa mbalimbali zikiwemo za uwekezaji hapa nchini.

Mhe. Profesa Ndalichako amesema hayo leo tarehe 22 Oktoba, 2022 jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa jengo la kitega uchumi la Mzizima Tower linalomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

“Tunafahamu namna ambavyo Mhe. Rais wetu Samia Suluhu Hassan anafungua fursa za Uwekezaji, kwa hiyo nanyie NSSF mnatengeneza mazingira ambayo wawekezaji watakapokuja nchini watapata sehemu ya kuishi na sehemu ya kufanya biashara zao,” amesema Mhe.Profesa Ndalichako.

Mhe. Profesa Ndalichako amesema kupitia uwekezaji huo wa mradi wa Mzizima Tower inadhihirisha kuwa NSSF inaunga mkono juhudi ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaendana na kazi kubwa ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa anaifanya ya kufungua uchumi wa nchi, kuweka mazingira mazuri kwenye sekta binafsi na kukaribisha wawekezaji nchini.

“Tumeshuhudia kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambavyo imefungua fursa na hivi sasa wawekezaji kutoka Mataifa mbalimbali wanakuja nchini, hivyo bado tunahitaji majengo mengi zaidi ya biashara ikiwemo hoteli ya namna hii,” amesema.

Amewasihi NSSF kuendelea kufanya kazi kwa wakati ili Serikali iweze kuona manufaa ya mradi huu, pia na fedha za wanachama ambazo zimewekezwa kupitia mradi huu zianze kurejeshwa, lakini kubwa zaidi mtengeneze ajira kwa vijana ambapo mradi huo ukianza kufanya kazi ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinaweza kufika 1000.

Mhe. Profesa Ndalichako pia amepongeza Bodi ya Wadhamini, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na Managementi kwa kazi kubwa mnayofanya hasa ya kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zimejitokeza katika mradi huu ambao utakapokamilika utachagiza maendeleo ya Taifa na wananchi kwa jumla.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema maendeleo ya ujenzi wa mradi huu yanaendelea vizuri.

Kwa upande wake, Msanifu wa Majengo ya Mzizima Tower, Kaisi Kalambo amemueleza Mhe. Waziri Profesa Ndalichako kuwa maendeleo ya mradi huo yamefikia asilimia 88 na kuwa jengo hilo likikamilika litatumika kwa matumizi ya ofisi, hoteli na makazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (katikati) akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa uwekezaji wa jengo la Mzizima Tower lililopo jijini Dar es Salaam, linalomilikiwa na NSSF.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, akiendelea kukagua maeneo mbalimbali katika mradi wa uwekezaji wa jengo la Mzizima Tower, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea maendeleo ya mradi wa uwekezaji wa jengo la Mzizima Tower jijini Dar es Salaam, linalomilikiwa na NSSF.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba akitoa maelezo mafupi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, (hayupo pichani), mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea mradi wa uwekezaji wa jengo la Mzizima Tower jijini Dar es Salaam, ambalo linamilikiwa na NSSF.
Msanifu Majengo, Kaisi Kalambo, akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, (hayupo pichani) kuhusu maendeleo ya mradi wa uwekezaji wa jengo la Mzizima Tower jijini Dar es Salaam,w ambalo linamilikiwa na NSSF.