December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mwambe aineemesha Masasi, agawa pikipiki 25

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Mtwara

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Mbunge wa Masasi, Geoffrey Mwambe, azidi kuling`arisha jimbo hilo mara baada ya kugawa pikipiki 25 kwa kikundi cha bodaboda kilichopo Wilayani hapa.

Wazir Mwambe amegawa pikipiki hizo wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Uwanja wa Fisi, Masasi mjini na kuwasisitiza bodaboda hao kuwa mpango huo utakuwa endelevu kwa kuwa wahitaji wa pikipiki hizo wamekuwa wengi na kuahidi kufanikisha upatikanaji wa zingine kwa siku za usoni.

“Natambua maombi ya walioomba pikipiki yalifika mia mbili (200), lakini tulipitia tukaona wanaokidhi vigezo ni 25, hivyo niwaahidi mchakato huu hautoishia hapa bali utakuwa endelevu kwa awamu nyingine”, alisema Bw. Mwambe.

Amesema pikipiki zimetolewa kwa njia ya mkopo nafuu ambao umelenga kuwawezesha bodaboda hao na kuwasisitiza kufanya marejesho kwa wakati na kutokuzitumia pikipiki kufanyia uhalifu.

“Pikipiki hizi zinakwenda kuwa sehemu ya ajira kwa baadhi yenu, lakini nawasihi msisahau kufanya marejesho na kutokuzititumia kufanya vitendo viovu vya uhalifu”, alisema Waziri Mwambe.

Mwambe aliongeza kuwa; “Nia na matumaini yangu ni kuwatumikieni nyinyi ambao mumeonesha imani kubwa kwangu na ninawakikishia kuwa, serikali imejidhatiti kuhakikisha inatatua kama sio kumaliza kabisa changamoto zinazotukabili ikiwemo maji, afya, elimu na miundombinu”.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Claudia Kitta alimpongeza Mbunge huyo kwa jitihada zake za kufanikisha upatikanaji wa bodaboda hizo ambazo zimefungua ajira kwa vijana ishirini na tano kwa wakazi hao.

“Kwa dhati kabisa nakupongeza Mbunge, kazi unayoifanya inajionesha na tukio hili ni sehemu tu ya alama yay ale mazuri na yenye manufaa kwa wakazi wa Masasi”, amrsema Bi Kitta.

Naye Mwenyekiti wa Bodaboda hao, Selemani Ajali amemshukuru mbunge huyo kwa kufanikisha mikopo ya pikipiki hizo ambao una masharti nafuu kwao kuweza kuyamudu.

“Kwa niaba ya bodaboda wenzangu, napenda kutoa shukrani zetu kwako kwa kutusaidia kufanikisha mpango huu na ninakuahidi tutazitumia pikipiki hizi kujihimarisha kiuchumi na kuondokana na umaskini”, amrsema, Ajali.

Ameongeza kuwa wao kama vijana na wakazi wa Masasi wataendelea kumuunga mkono mbunge huyo kwa kuwa matunda ya uwakirishi wao bungeni yanazaa matunda kwa kuwa kero mbalimbali zimeanza kutatuliwa jimboni hapo.

“Sisi kama vijana tunakuahidi kukuunga mkono na tuna imani kubwa kwako kwa kuwa umeshaonyesha nia njema uliyonayo kwetu”.

Waziri Mwambe ameendelea kuonyesha dhamira ya dhati kwa ajili ya wananchi wa Masasi huku akiainisha kuwa serikali itaendelea kuvipa kipaumbele sekta muhimu kama vile maji, afya, elimu, umeme na miundombinu katika jimbo hilo.