Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Umoja wa Afrika (AU) ulioanza leo Jijini Malabo, Equatorial Guinea.
Kufanyika kwa mkutano huo ni utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika tarehe 6 – 7 Februari 2022 Jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa Kisekta wa Mawaziri wanaoshughulika na Wakimbizi, Wahamaji na Majanga ya Kibinadamu uliofanyika kuanzia tarehe 23 – 24 Mei, 2022 Jijini Malabo.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine, jukumu lake kubwa ni kuandaa Mkutano Maalum wa 16 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu majanga ya kibinadamu pamoja na masuala ya mapambano dhidi ya ugaidi na mabadiliko ya serikali yasiyozingatia Katiba unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 – 28 Mei, 2022 Jijini Malabo.
Akiongea wakati wa Ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bw. Moussa Faki Mahamat alisema kuwa mkutano huo ni mahsusi katika kujadili changamoto mbalimbali za majanga ya kibinadamu pamoja na mapambano dhidi ya ugaidi na mabadiliko ya Serikali yasiyozingatia katiba
“Mkutano huu unafanyika wakati Afrika linapita katika changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na za majanga ya kibinadamu,” alisema Bw. Mahamat
Aidha, Bw. Mahamat aliongeza kuwa ugaidi bado ni changamoto na mabadiliko ya Serikali yasioyofuata misingi ya katiba ambayo yametokea miaka ya hivi karibuni yamerudisha nyuma taratibu za kidemokrasia katika chaguzi katika Bara la Afrika.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best