November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Idara na Taasisi za utafiti na elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingira.

Pia amezitaka Idara na Taasisi za Serikali zitumie matokeo ya tafiti hizo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Kitaifa.

Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akifungua Mkutano wa Afya Moja Novemba 4, 2024 Jijini Arusha ambapo amesema Taasisi zote zinazohusika na masuala mtambuka katika afya ya jamii, wanyama na mazingira zitenge fedha na kuweka katika mipango ya taasisi hizo afua za kuthibiti magonjwa ya kizoonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, magonjwa yasiyoambukiza, mabadiliko ya tabia nchi, na usalama wa chakula.

“Wizara za kisekta, na Mamlaka za Serikali za Mitaa, andaeni mipango kazi na taratibu za usimamizi kwa ajili ya utekezaji wa mbinu ya Afya Moja kwa kuzingatia miongozo iliyopo ambayo imeweka bayana majukumu ya wadau wote aidha Mamlaka za Serikali za Mitaa fanyeni vikao vya mara kwa mara, kufanya tathmini ya utekelezaji wa pamoja wa afua mbalimbali, kwa kufanya hivyo changamoto zitajulikana mapema na kupatiwa ufumbuzi”.amesema Majaliwa

Aidha amesema tafiti zinaonesha kuwa, duniani kote takribani visa bilioni moja vya ugonjwa pamoja na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu aidha, zaidi ya asilimia 75 ya vimelea vipya 30 vya magonjwa vilivyogunduliwa katika miongo mitatu iliyopita, vimetoka kwa wanyama.

“Kwa mujibu wa taarifa na takwimu zilizopo, Taifa la Tanzania kama mataifa mengine duniani limekuwa likikumbwa na magonjwa hayo, Kama mtakumbuka, mnamo mwaka 2017 wataalam wetu kutoka sekta mbalimbali waliainisha magonjwa ya zoonotiki yanayopewa kipaumbele hapa nchi kwetu ambayo ni kichaa cha mbwa; kimeta; malale; brusela; homa ya bonde la ufa; homa ya mafua; na magonjwa yanayosababishwa na virusi vya ebola na Marburg”amesema Majaliwa

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga akieleza kuhusu mkutano huo amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu shughuli za Serikali ikiwemo la menejimenti ya maafa ambapo katika hatua hii Dhana ya Afya Moja inaendelea kupewa kipaumbele hususani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwani suala hilo linagusa sekta nyingi.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema matatizo mengi yanayoathiri afya ya binadamu kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 60 huanzia kwa wanyama, mimea pamoja na mazingira, hivyo dhana ya Afya Moja ndiyo njia pekee ya kukabiliana nayo na kuyadhibiti matatizo hayo.

“Katika kufanikisha dhana ya afya moja Wizara yangu iko tayari na itaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na sekta zenye dhamana ya afya ya Binadamu, Afya ya Mimea pamoja na Mazingira katika kutekeleza dhana hii. Washirika wa maendeleo wamekuwa wakishiriki na sisi bega kwa bega katika kukuza uelewa na ushiriki kwenye dhana hii,”amesema Ulega