January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Majaliwa azindua mpango wa mbolea bure

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Dar

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha mbolea ya bure inayotolewa na kampuni ya Yara Tanzania inawafikia wakulima waliolengwa na mpango huo kwa wakati ili kwenda sambamba na maandalizi ya msimu wa kilimo mwaka 2020/2021.

Uzinduzi wa mpango huo wa ugawaji mbolea tami 12,500 iliyotolewa na
kampuni ya Yara jijini Dar es Salaam jana ni sehemu ya
kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inapiga hatua na kutoa mchango
stahiki katika kuinua uchumi na kuongeza kipato cha mkulima mmoja
mmoja hapa nchini.

“Nachukua fursa hii kuipongeza kampuni ya Yara kwa kujitoa kwake
kuchangia kwenye kukuza sekta ya kilimo kwa kutoa mbolea bure kwa
wakulima zaidi 83,000,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema ni muhimu watendaji wa Serikali wakashirikiana na kampuni ya Yara kutimiza lengo la kuwafikishia mbolea wakulima kwa wakati na bure kama ilivyopangwa.

“Watendaji wasiwe kikwazo katika utekelezaji wa mpango huu ambao
una lengo la kuwanufaisha hasa wakulima wadogo ili kuongeza uzalishaji wa mazao nchini,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa makamuni mengine yanayojihusisha na sekta ya kilimo kuiga mfano huu wa Yara kuboresha sekta kwa kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (watatu kulia) akinyanyua bendera kuashiria uzinduzi rasmi wa ugawaji wa mbolea bure kwa wakulima wadogo nchini uliofanyika ofisi za kampuni ya Yara Tanzania jijini Dar es Salaam na kumeratibiwa na Kampuni hiyo kupitia mradi wa Action Africa ambapo zaidi ya tani 12,500 zitatolewa. Wapili kulia ni Balozi wa Norway Nchini, Elisabeth Jacobsen na Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yara Tanzania, Winstone Odhiambo.

“Natumia nafasi kuyataka kampuni mengine kujitoa ili kusaidia sekta hiyo hususani kwenye suala la pembejeo na zana za kilimo kwa kuwa kilimo ni sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania,” amesema Majaliwa

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema wizara yake pamoja na mamlaka za uthibiti zimejiridhisha kuwa mbolea ya Yara inafaa kwa matumizi kulingana na mazingira ya nchi yalivyo na hivyo itachochea kuongeza uzalishaji wa mazao ya mahindi na mpunga.

“Taratibu za kufanya ithibati ya mbolea hii zimezingatiwa hivyo
tunaimani zitachangia katika kuongeza ubira na uzalishaji wa mazao
nchini,” amesema Hasunga

Alisema Serikali itaendelea kwa kuhamasisha na kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya matumizi ya mbolea na mbegu bora na viua tirifu zinavyofaa kulingana na ardhi yetu ili kuongeza uzalishaji ili nchi ijitosheleze kwa chakula.

“Serikali imejipanga kuhakikisha masoko ya mazao yanapatikana ili
mkulima aweze kufaidika na shughuli yake jambo litakalo chochea ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla,” amesema Hasunga

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza jambo katika uzinduzi wa rasmi wa ugawaji wa mbolea bure kwa wakulima zaidi ya 83,000 nchini uliofanyika ofisi za kampuni ya Yara Tanzania jijini Dar es Salaam na kumeratibiwa na Kampuni hiyo kupitia mradi wa Action Africa ambapo zaidi ya tani 12,500 zitatolewa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yara Tanzania, Winstone
Odhiambo alisema mpango huu ni jitihada za kampuni mama kutoka Norway kuhakikisha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinajitosheleza kuzalisha chakula.

“Mpango huu wa usambazaji mbolea bure unafanyika kupitia mradi maalum ujulikano kama ‘Action Africa’, “ alisema Odhiambo na kuwataka wakulima hapa nchini kuchangamkia fursa hiyo kugawiwa mbolea bure.