June 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu kuzindua Kampeni ya msaada wa kisheria Dar

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonlin,Dar

MKUU wa Mkoa Dar es Salaam, Albert  Chalamila, amesema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa,anatarajiwa kuzindua kampeni ya Msaa wa Kisheria ya (Mama Samia Legal Aid Campaign) Wilaya ya Temeke Juni 16 mwaka huu Viwanja vya Maturubahi Mbagala.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Juni 13,2025,Chalamila amesema dhumuni la kampeni hiyo kuwasaidia watu wa Mkoa Dar es Salaam wenye changamoto za kisheria za mirathi,ukatili wa kijinsia,migogoro ya ndoa.

“Kutokana na changamoto mbalimbali za Kisheria zinazowakabili wananchi hasa wa Dar es salaam,Wizara ya Katiba na Sheria ,kupitia kampeni “Mama Samia Legal Aid”litaendesha zoezi la kutoa msaada wa kisheria siku kumi mfululizo kuanzia Juni 16 “amesema Chalamila.

Aidha Chalamila amesema mara baada uzinduzi wa kampeni hiyo baadae itafanyika kila wilaya kwa utaratibu maalum wa ratiba ili wananchi waweze kutumia fursa hiyo kutoa changamoto zao za kisheria,zikiwemo mirathi,migogoro ya ardhi,ndoa, uandishi wa wosia,pamoja na nyingine zitakazotolewa na wataalam wa sheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria,Esther Msambazi,amesema
kutokana na changamoto hizo zilizopo katika jamii kuhusiana na uelewa wa masuala ya kisheria,Serikali iliamua kuanzisha kampeni hiyo ya Mama Samia Legal Aid ili kusaidia wale ambao hawana uwezo wa kupata huduma hizo.

Msambazi amesema kampeni hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwa wananchi ambao wengi wao wanashindwa kupata huduma za kisheria kutokana na kipato au kutokuwa na uelewa juu ya masuala ya hayo.

“Hadi sasa Wananchi mil.2 wamefikiwa na huduma hiyo katika mikoa mitano ya Zanzibar,na 26 ya Tanzania Bara”amesema Msambazi.