Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua studio za kidigiti za redio ikiwa ni sehemu ya mradi wa maboresho ya studio za redio, televisheni na mitandao ya kijamii za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Uzinduzi wa studio hizo za kidijiti za redio na mitandao ya kijamii kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) umefanyika Jijini Dar es salaam leo Aprili 20, 2024
Amesema uzinduzi wa mitambo hiyo ya TBC umezingatia awamu ya tatu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano ambao umeanza mwaka 2021-2026 na mpango huo umeainisha vipaumbele katika utekelezaji wa miundombinu ya TBC ikiwepo upanuzi wa usikivu wa redio, ununuzi wa mitambo na vifaa vya redio na televisheni.
Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ibara ya 125, kifungu F imeweka mazingira kwa serikali kuimarisha Shirika la Utangazaji la taifa ikiwa kuwepo na ubora wa usikivu na kuanzisha kituo kikubwa cha utangazaji Makao Makuu ya Nchi, jijini Dodoma na kwenye kanda zote za shirika hilo.
“Serikali imekuwa ikitekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa mafanikio makubwa na imejikita katika kufanya maboresho kwa vyombo vya habari na kwa sasa serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha TBC Dodoma kitakachogharimu sh. bilioni 54 na kitakamilika Februari, mwakani ,” amesema
Aidha Majaliwa alilitaka shirika la TBC kuimarisha umoja na ubuniufu walionao kwani hiyo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo huku Wizara ikitakiwa kuendelee kulisimamia vizuri shirika kwa kuimarisha utendaji kazi wake kwa kushirikiana nalo ili kila mmoja awajibike katika mipango iliyowekwa katika kuimarisha shirika kwa viwango vya juu.
Pia aliishauri bodi ya shirika hilo kupeleka mapendekezo muhimu ambayo wameyaona kwa ubunifu wanaouweka kuwa yataliwezesha shirika kusikika kikamilifu katika maeneo yote ndani na nje ya nchi.
Pia alilitaka shirika hilo kuweka mkakati wa kuandaa maudhui kwa kuimarisha maadili, kudumisha mila na desturi za Watanzania bila kusahau kudumisha muungano na kukuza uzalendo.
Pia aliwataka waandae makala zitakazoelezea ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Naye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye amesema sheria ya TBC imekamilika na imepita kwenye ngazi zote na sasa ipo katika hatua ya Baraza la Mawaziri kabla ya kupelekwa bungeni.
“Sheria ya TBC ipo katika mchakato mzuri, tumepitia michakato yote na sasa ipo katika hatua ya kikao cha mawaziri, ikipitishwa itawezesha TBC kuwa na uwezo wa kujiendesha yenyewe bila kusubiri ruzuku kutoka serikalini,” amesema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt Ayub Rioba amesema TBC ni moja ya vyombo vya mfano Afrika vilivyofanya mageuzi makubwa.
Amesema shirika hilo ili kutoa huduma bora kwa jamii wametanua usikivu ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2006 hali ya usikivu ilikuwa asilimia 54 na miradi ikikamilika itafikia asilimia 92 kwani hadi mwakani watakuwa wameyafikia maeneo yote nchini .
Pia amesema wamefanikiwa kuimarisha maudhui mtandaoni ambao kiasi cha sh. bilioni 5.7 kitatumika katika mradi huo nchini.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi