May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Abdulla: Anayeulalamikia muungano akili yake haiko timamu

Na Mwandishi wetu TimesMajira Online

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema ukiona mtu anaulalamikia Muungano ambao umewekwa na waasisi basi akili yake haiko timamu anahitaji huduma ya kimatibabu kwa sababu sera na miongozo iliyowekwa inafuatwa.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwaunga mkono viongozi ili waweze kuendelea kuleta maendeleo katika nchi na pia kuna haja ya wao
kuendelea kujifunza historia ya nchi na kujua umuhimu wa muungano.

Makamu Abdulla amesema hayo katika Uzinduzi wa Maonesho ya Biashara miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika Viwanja vya Mnazi Mmoja , Dar es Salaam yaliyoandaliwa na
Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

“Leo hii mtanzania ana haki ya kwenda kokote akafanya kitu bila kubuguziwa na pia watu wanaona kutoka pande zote mbili.
Huu ndiyo umoja wa waasisi wetu waliyouweka kwa faida kubwa, mtanzania mwenye akili hawezi kutoa maneno mabaya kuhusu muungano ukimuona mtu ana lalamika muangalia akili yake iko timamu,”

“Kama haiko timamu basi mawaziri wetu wa afya watatakiwa kumshughulikia kwa sababu hayuko sawa, lakini kama wana hoja na ushauri basi wazilete mezani zishughulikiwe kikamilifu sio kuuzungumzia vibaya Muunganokwa maneno mabaya,”amesema Makamu Abdulla

Pia, amesema kutokana na muungano unavyoendesha hivi sasa hakuna malalamiko yoyote,watu wanatakiwa wajifunze wajue Muungano wao vizuri kupitia maonesho haya, waendelee kuulinda na kuudumisha kwa gharama yoyote.

“Ni wajibu wa kila watanzania kulisimamia jambo hili kwa faida yetu na kwa vizazi vijavyo, kwa sababu vijana wanatakiwa kuendelea kufundishwa juu ya Muungano na uzalendo hasa kwa wanafunzi wetu,”amesema

Aidha, amesema ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi umeongezeka kwa pande zote mbili za Muungano na hilo inatokana na sera na miongozo iliyowekwa inayorahisisha kuondoa changamoto za kiutendaji na upatiakanaji wa huduma kwa wananchi.

“Viongozi na wananchi niendelee kuwakumbusha kwamba Muungano umedumu kwa miaka 60, kwa hiyo tuendelee kuudumisha na kuulinda ili vijana wetu wauendeleze,”amesema

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Khamis amesema utamaduni huo ni kielelezo tosha cha Muungano, watanzania wote wanatakiwa kutafakari yalifanywa na waasisi wa nchi hii kwa misingi waliyoiyacha na kwamba imeendelea kuimarika.

Amesema katika maonesho hayo wananchi watapata fursa ya kujua masuala ya muungano kwa kujua chimbuko la msingi na nini siri ya mafanikio ya muungano huo kwa kufika katika viwanja hivyo.

“Muungano umetuletea mambo makubwa ,uhuru wa kuishi kwa amani na uchumi umeimarika kati Tanzania bara na Zanzibar,”amesema

Kwa upande wake, Meneja Ukuzaji Biashara wa TanTrade, Mohamed Tajiri amesema uzinduzi huo wameweza kupata Abdulla hiyo yote ni katika kudumisha muungano na kuonesha kwamba wanadhamira safi baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema kuwa kuna mambo bayana ambayo ameyaanisha Abdulla yanajenga umoja wetu, lengo mahususi ya maonesho hayo kuweza kupata fursa ya watembeleaji lakini pia na zile taasisi za muungano na binafsi na taasisi za umma ziweze kushiriki na kutoa nafasi ya kuielezea jamii na uuma wa watanzania kuhusiana na huduma zinazotolewa.

“Lakini vile vile kuna taasisi ambazo zinaweza kutoa huduma hapahapa ikiwepo utoaji wa pasipoti, Idara ya Uhamiaji Zimamoto, Rita Nida na Benki Kuu na TanTrade tupo hapa katika kuelimisha wananchi jinsi yaka kazi tunazofanya na ukuzaJi wa biashara nje ya nchi,”amesema