January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu ataka Mbeya Tulia Marathon kuongeza wigo

Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa taasisi ya Tulia Trust kupanua wigo wa kualika nchi jirani za Malawi , Zambia , Congo , Msumbiji katika mashindano ya Mbeya Tulia Marathon .

Majaliwa amesema hayo Mei 11 ,2024 wakati wa kilele cha mbio za Tulia Marathon katika uwanja wa Sokoine ambayo yamejumuisha nchi za jirani za Kenya,Uganda pamoja na wanariadha wa ndani na nje ya nchi ambapo Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi.

“Kutokana na umuhimu wa mbio hizi oneni namna ya kupanua mialiko mpaka nchi jirani mfano Malawi, Zambia , Msumbiji, Congo ,leo tuna Kenya na Uganda lakini tunaweza kupanua wigo twende Rwanda na Burundi zitangazwe kuanzia Januari 2025 tarehe fulani mwezi wa tano kutakuwa na mbio za Tulia Marathon zitangazwe na fursa zake ili kampuni , wakimbiaji ,washangiliaji waje kukutana hapa,”amesema Waziri Mkuu.

Aidha amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana na taasisi hiyo ili iendelee kunufainisha Wilaya na Halmashauri zote katika Mkoa wa Mbeya.

“Wananchi michezo ni afya,tutenge muda wa kufanya mazoezi tuache ubize kwani mazoezi ni kinga, ukishiriki huwezi kupata magonjwa yasiyoambukiza kwani yamekuwa yakiliingizia taifa gharama kubwa na kupoteza nguvu kazi,twende tufanye mazoezi tuwe na afya njema magonjwa“amesema Majaliwa.

Hata hivyo amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha watanzania kujishughulisha kupitia mazoezi na michezo mbalimbali,kupenda michezo , kuimarisha vikundi vya michezo mfano mpira wa miguu , ngumi ,riadha, mbio za magari na pikipiki.

Akizungumzia kuhusu Wizara ya Maliasili na Utalii Majaliwa ameitaka Wizara hiyo kutumia fursa ya mbio hizo kutangaza utalii wa Mkoa wa Mbeya kwa vivutio vya utalii vilivyopo mkoani humo .

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge Dkt. Tulia amesema wana mpango wa ujenzi wa miundombinu ambayo itawaweka vijana ambao wanataka kukimbia mbio fupi na ndefu wawe na kambi sehemu ambayo itawazesha kufanya mazoezi .

“Litafutwe eneo zuri Naibu Meya hapa Mbeya kwa sababu jambo linaanzia hapa tunahitaji hekta 15 kwa ajili ya kituo hicho ambacho kitasaidia kukuza vipaji vya vijana wetu wanaopenda riadha,”amesema Dkt. Tulia.