Afungua wiki ya maji kwa kuzindua mradi wa Bilion 70
Na Mwandishi wetu, Timesamajira Online
Hatimaye wakazi wa Tegeta A, Wazo, Goba, na Madale wameanza kufurahi kufuatia kuzinduliwa rasmi kwa mradi mkubwa wa kusambaza maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo uliotekelezwa na Serikali kwa ufadhiki wa Benki ya Dunia unaotegemea kunufaisha wananchi takribani 450,000.
Mradi huu ni mojawapo ya mradi uliokuwa unasubiriwa kwa muda mrefu na wakazi wengi hasa wa Tegeta A, Mivumoni, Goba, Madale na Wazo ambao wamekosa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameipongeza DAWASA kwa kutekeleza mradi kwa ufanisi na kwa wakati, kukamilika kwa mradi kunatoa nafasi kwa wananchi kuanza kunufaika na maji.
Amesema kuwa kwa sasa kazi iliyopo ni kuhakikisha wananchi wote wanafanyiwa maunganisho ya maji ili kila mmoja aone manufaa ya mradi huu nyumbani kwake.
“Serikali inatambua changamoto ya maji iliyokwepo kwenye maeneo haya, na ndio maana Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alifanya uamuzi wa dhati wa kusukuma utekelezaji wa mradi huu ili wananchi mpate maji,” ameeleza Mhe Kassim Majaliwa.
Mameneja wa mikoa ya kihuduma DAWASA ongezeni nguvu katika kusambaza maji mitaani, nimepita kwenye kituo cha kusukuma maji na kwenye tenki, maji yanashuka yenyewe bila kusukumwa na umeme, hivyo hamna sababu ya kushindwa kusambaza maji kwa wananchi,” amesisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Mbali na hapo, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi kuwa makini na kutokukubali mtu yeyote kuwalaghai na kutaka rushwa kwa ajili ya kuunganishiwa maji, utaratibu wa Serikali wa kuunganisha watu maji uzingatiwe na kufuatwa ipasavyo.
“Niwatake wananchi kuwa na tabia ya kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na mazingira, kuharibu Mazingira ni kuhujumu.
“Serikali kwa pamoja inaendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta vyanzo mbalimbali vya maji ili kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote,” amesema Mhe Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzindua rasmi maadhimisho ya wiki ya maji Duniani inayoanza Machi 16 – 22.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso ameipongeza DAWASA kwa kufanikisha utekelezwaji wa mradi mkubwa uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu. Kazi ya kufanya sasa ni kuharakisha wananchi wapate maji.
Pia Waziri Aweso amekemea tabia ya kubambikiza bili kwa wateja na kuwataka DAWASA na Mamlaka zote nchini kuwa makini katika usomaji na utoaji wa bili sahihi na kwa wakati kwa wateja.
“Pasiwepo na usumbufu katika kuwaunganisha wananchi na huduma ya maji, ndani ya siku 14 za kazi mwananchi aliyekidhi vigezo apewa huduma ndani ya muda,” amesisitiza Mhe Aweso.
Amebainisha kuwa rasilimali zilizopo nchini ni toshelevu kuweza kutoa huduma kwa wananchi wote, hivyo pasiwepo na usumbufu katika kutoa huduma.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa mradi huu umetekelezwa kikamilifu ukihusisha ujenzi wa matenki makubwa matatu ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita milioni 5 kila moja, ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji, ulazaji wa bomba kubwa la 16 la kusafirisha maji kwa umbali wa kilomita 1,252. Mradi umetekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kwa kiasi cha bilioni 70.
Nae mkazi wa Tegeta A Bi Mwanahija Hassan amesema kuwa kutoka kwa maji ya bomba kwake ni faraja maana hajawahi kupata maji ya bomba kabisa, amekuwa akitumia maji ya chumvi na ya kununua kwa gharama kubwa.
Anaishukuru Serikali kwa jitihada zilizofanyika za kufikisha maji kwao, kwani sasa hatateseka tena kufuata maji mbali.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua