Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Songwe
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim Majaliwa amemuelekeza Mganga mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Songwe, kuhakikisha huduma za afya kwenye mkoa huo, Wilaya na Halmashauri zinaimarika kwa kupata huduma iliyo bora
Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo jana Mkoani Songwe alipokuwa akizungumza na wananchi wa mkoani humo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa songwe Katika Kata ya Asamba, Wilayani Mbozi.
“Hapa tulipata tatizo tulipoanza kuleta vifaa baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu wakawa na tamaa na hivyo vitu na mmoja tukamkamata akiwa anaiba kifaa muhimu sana cha kupima magonjwa ya wakina mama ya ndani ya tumbo, alikua anakiiba akauze, na sasa tumefanya mabadiliko ya mganga mkuu”
“Mganga mkuu umeletwa hapa uhakikishe huduma za afya kwenye mkoa huu zinaimarika, Si tu hospitali hii ya Mkoa na hospitali za makao makuu ya Wilaya zote, Hospitali Makao makuu ya Halmashauri zote, vituo vya Afya vyote, na zahanati zote, kila mahali huduma lazima iende vizuri”
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa aliwaagiza wakuu wa Ilaya na wakuu wa Idara wote kwenda kwa wananchi vijijini kufanya mikutano kusikiliza kero zao ili ziweze kufanyiwa kazi.
“Wakuu wa Wilaya, nendeni kwa wananchi vijijini mkawasikilize matatizo yao, tuyaratibu, tuwahudumie, serikali hii imejidhatiti kwaajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo iteni mikutano ya kero nendeni na wakuu wa idara sikilizeni kero zao” Alisema Waziri Majaliwa na kuongeza kuwa
“Hospitali hii inayojengwa hapa mkoani Songwe ni ya kimkakati, mkoa huu unapakana na nchi jirani ya Zambia na Malawi, ndugu zetu wa Zambia na Malawi hawana huduma kubwa kama inayotolewa hapa, maana yake na wao watakuja hapa mbozi kutibiwa, kwahiyo hapa tuna utalii wa kimatibabu”
Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali ya awamu ya sita iliyo chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo imara ambapo amewapa malengo ya kuwahudumia wananchi hasa katika maeneo yanayowagusa wananchi ikiwemo Elimu, Afya, Maji, Uboreshaji wa Barabara, Kilimo na Sekta ya maji ambapo amesisitiza kuwa uwepo wa Wakala wa maji Vijijini (RUWASA) ni kuhakikisha kuwa huduma ya maji safi na salama inafikia hadi maeneo ya vijijni.
“Mkoa huu wa Mbozi unakwenda kwa Kasi sana na lazima muendelee kujipanga vizuri, na serikali yenu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawaunga mkono, na kwasababu Rais anawaletea fedha nyingi ambapo mpaka sasa mkoa huu zimeshaingia zaidi ya Bilioni 579 kwaajili ya miradi mbalimbali”
“Wananchi serikali yenu ipo imara, Rais wetu ambaye ametupa malengo ya nini tufanye kuwahudumia nyie malengo yake bado yapo palepale kwa kuwahudumia nyie, na amesisitiza sana kwamba huduma mnazitakiwa kuzipata ni Yale maeneo yote ambayo ukiamia tu unaanza kuyagusa ikiwemo elimu, Afya, Maji, kuimarisha Barabara na Kilimo” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili