February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Lukuvi akutana na wadau sekta binafsi



Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu,William Lukuvi amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa Sekta binafsi katika kikao kilichoratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Kikao hicho kilichofanyika Februari 18, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es salaam, kilicholenga kujadili ushiriki wa Sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara kwa kuangalia fursa za uchumi ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati ya kutumia fursa hizo vizuri na kushauri Serikali katika maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Akizungumza katika kikao hicho Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Angelina Ngalula amesema Sekta binafsi ndio injini ya kusukuma uchumi, inayochukua fursa zote zinazofunguliwa na serikali kama mabadiliko makubwa ya sheria na taratibu, kutolewa kwa tozo inalenga kutoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza na kupata mafanikio.

“Katika Kipindi cha Miaka Minne ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani umefanya kazi kubwa sana katika uwekezaji wa miundombinu ambayo imesaidia katika kuchochea biashara,” alieleza Angelina.

Akichangia kuhusu Sekta ya Kilimo  Jacqueline Mkindi amesema sekta ya kilimo na mifugo imenufaika sana kwa sababu ya nguvu ya serikali kutangaza diplomasia ya uchumi na kueleza kuwa umeongeza uhitaji wa bidhaa za Tanzania nje ya Nchi.