Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini, Angellah Kairuki ametoa rai kwa Watanzania kuwekeza katika sekta ya mafuta ya kula kwa kuzingatia uhitaji na soko lililopo ndani na nje ya nchi.
Ametoa rai hiyo alipotembelea na kukagua kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula cha SUNSHINE kinachozalisha mafuta yanayotengenezwa kwa kutumia malighafi ya alizeti yanayoitwa Sunbelt kilichopo katika eneo la Zuzu jijini Dodoma.
Akiwa katika ziara hiyo, yenye lengo la kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji nchini.Waziri Kairuki alipongeza uwekezaji katika kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 25 kwa siku na kilichowekeza zaidi ya shilingi Bilioni 230.
Amengezea kuwa, ni vyema watanzania wakaendelea kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la alizeti kwa kuzingatia uhitaji mkubwa wa mafuta ya kula nchini kwani nchi imekuwa ikipoteza zaidi ya shilingi bilioni 443 kwa mwaka kwa kuagiza mafuta nje ya nchi.
Aidha, Waziri amebainisha kuwa uwekezaji huo ni miongoni mwa fursa muhimu na kuwataka wenye uwezo kulima zao hilo kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo kwa vile zao hilo linastawi katika ukanda huo.
Ametumia fursa hiyo kuendelea kuwasihi wataalam wa masuala ya kilimo kutoa elimu kwa umma kuhusu kilimo bora cha zao hilo ili kuwa na utaalam wa kutosha kuhusu kilimo cha zao hilo ili kutumia mbinu za kisasa na zenye kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Meneja Biashara na Maendeleo wa kiwanda hicho, Krishna Urs alieleza changamoto wanayokabiliana nayo ni uhaba wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji na kuendelea kutoa wito kwa wadau kuitumia fursa ya kilimo cha zao hilo ili kuendana na mahitaji halisi.
Naye Afisa Viwango wa kiwanda hicho, Upendo Mganda alipongeza uwekezaji huo kwa kuwa, umesaidia kutoa ajira na vibarua kwa wananchi walio wengi.
“Tunashukuru uwepo wa kiwanda umetusaidia kupata ajira na wazawa wameweza kuuza malighafi zao kiwandani hapa kwa bei yenye tija,” alisema Upendo
Aidha aliongezea kuwa, ni kiwanda chenye tija kwa kuzingatia uwezo wake wa uzalisha tani 24 hadi 25 kwa siku na kinafanya vizuri sokoni kwa kuzingatia kuwa mafuta yanayozalishwa hayana kemikali zenye athari kwa watumiaji.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi