Na Mwandishi Wetu, Iringa.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Kongani ya Ihema kwenye Ushoroba wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOTna kuwataka wakuu wa mikoa katika eneo hilo (Iringa, Njombe na Mbeya) kushirikiana na wawekezaji kwa karibu kutatua changamoto ili kuongeza uzalishaji.
Akizungumza kwa nyakati tofauti alipotembelea kiwanda kuzalisha maziwa cha ASAS Dairies Farm Limited, GBRI Solutions Tanzania Ltd na Farm for the Future, Kairuki amesema uwekezaji katika eneo hilo umekuwa na mchango mkubwa kwa kuongeza mnyororo wa thamani za mazao pamoja na kuinua sekta ya maziwa.
“Wakuu wa mikoa katika ushoroba wa SAGCOT ni vizuri wakashirikiana pia na kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwani uwekezaji huo umeshatoa matokea chanya kwa kubadilisha maisha watu na kuongeza kipato cha taifa,” amesema Kairuki ambaye yupo katika ziara ya kutembelea mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya ili kukagua na kujionea shughuli za uwekezaji pamoja na kuzungumza na wawekezaji katika mikoa hiyo.
Katika ziara hiyo Waziri ameipongeza SAGCOT pamoja na Ofisa Mtendaji wake Mkuu, Geoffrey Kirenga kwa kuwa mfano mzuri katika kuhamasisha uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji (TIC) na kuzitaka taasisi zingine kuiga mfano huo.
“Siyo jambo la kuficha kwani maeneo ya uwekezaji katika mikoa ya Iringa Mbeya na Njombe ni makubwa ni mazuri kwa shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo wakati umefika kwa wawekezaji kuendelea kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kujisajili TIC na unufaika na fursa za vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi,” amesema.
Kairuki amesema wakati umefika kuangalia miradi katika eneo zima la kongani ya ihemi ambayo bado haijasajiriwa TIC, ikasajiliwe ili mwekezaji aweze kunufaika na fursa za vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi zinazotolewa kwa mwanachama pekee.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli inatambua mchango wa uwekezaji wenu na ndiyo maana inaboresha miundombinu muhimu ikiwemo uwepo wa nishati ya umeme ya uhakika, barabara bora, upatikanaji wa maji safi, kuboresha mifumo ya mawasilino na upatikanaji wa huduma bora za mamlaka zinazosimamia masuala yanayohusu uwekezaji nchini.
Naye Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS, Fuad Abri ameipongeza Serikali kwa hatua madhubuti wanazozichukua kuhakikisha wanaboresha mazingira ya uwekezaji ikiiwemo miundombinu sambamba na kuanzisha Dawati la Sekta binafsi katika sekta ya ufugaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha GBRI Solution Tanzania Ltd kinachojiusisha na usindikaji wa matunda na mbogamboga, Hadija Jabiri, alisema mbali ya mafanikio anayoyapata amekuwa akikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kukidhi mahitaji ya soko la nje kwa kushindwa kufikisha mzigo sokoni kwa muda uliopangwa.
“Pamoja na mafanikio ninayoyapata bado nakumbana na changamoto zinazonikwamisha kukidhi mahitaji ya soko la nje, hususa kukosekana kwa miundombinu rafiki sambasamba na mitaji,” amesema Jabiri.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT Centre, Kirenga alisema kituo kitaendelea kunganisha nguvu kutoka sekta za umma na binafsi ili kutoa mchango stahiki wa maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo na mifugo hapa nchini.
“Kama wadau wa sekta ya kilimo,SAGCOT itashirikiana na serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi kufanikisha azma ya serikali ya Twamu ya Tano chini ya Dkt.John Magufuli kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ili kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda,” amesema Kirenga.
Alizishukuru taasisi na asasi mbalimbali ambazo zimekuwa mstari wa mbele kufanikisha shughuli na maendeleo ya kilimo na mifugo katika ushoroba wa SAGCOT ikiwemo Taasisi ya kuwezesha Sekta Binafsi katika Kilimo (PASS).
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme