Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) amewapongeza wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo utatuzi wa hoja 11 za Muungano ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Ametoa pongezi hizo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Makamu wa Rais cha kupitisha Bajeji ya Utekelezaji wa Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika leo Machi, 2022 jijini Dodoma
Akizungumza na wafanyakazi hao Dkt. Jafo aliwataka kuendeleza juhudi hizo ili wananchi wapate uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa Muungano na masuala ya Mazingira.
Pia, Dkt. Jafo alitoa pongezi kwa wafanyakazi wa Ofisi hiyo kwa kuwajibika ipasavyo katika sekta ya mazingira ikiwemo kusimamia kampeni mbalimbali zikiwemo ‘Soma na Mti’ ambayo inahusisha wanafunzi ngazi ya shule za msingi hadi vyuo kupanda miti na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa ya kijani.
“Kikubwa zaidi niwape moyo watumishi mmefanya kazi nzuri sana, sasa twendeni na spirit (moyo) tuendeleze upendo tulio nao maana bila upendo hakutakuwa na mafanikio,” alisisitiza Jafo.
Waziri huyo alisema vikao vya Baraza la Wafanyakazi ni muhimu katika kujadili masuala mbalimbali ya wafanyakazi kwa upana kwa kuzingatia haki, weledi ikiwa ni pamoja na kujadiliana changamoto za kiutendaji na hatua za kukabiliana nazo.
Aliongeza kuwa vikao hivyo vinalenga kudumisha utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja, bidii na maarifa ili kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Ofisi na Taifa kwa ujumla.
Hivyo aliwataka wafanyakazi kujadili suala la Bajeti kwa kina na ikiwa zipo changamoto zilizobainishwa mwaka wa fedha uliopita zijadiliwe ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi ili kurahisisha Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa fedha ujao.
“Ninaamini Bajeti hii imejikita katika kuwezesha, kudumisha Muungano wetu na imezingiatia masuala ya uhifadhi wa mazingira yetu unaosimiwa na Ofisi hii na pia niwaombe wajumbe boresheni utendaji kazi ili Ofisi hii iwe mfano wa Taasisi na Wizara zote katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa kuzingatia umuhimu wa Ofisi hii,” alisisitiza Jafo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa