October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Jafo awaasa wajumbe Bodi ya FCC kuwa waadilifu, waaminifu

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Selemani Jafo (Mb) amewaasa wajumbe wapya wa Bodi ya Tume ya Ushindani(FCC) kuwa waadilifu na Waaminifu katika majukumu yao ya kuitumikia taasisi hiyo na kuondoa maslahi binafsi na kufanya kwa maslahi ya umma.
 
Amebainisha hayo wakati anazindua bodi ya Taasisi hiyo Oktoba 4,2024 katika ukumbi wa Ofisi za Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
 
Mhe.Jafo amesema taasisi hiyo ni injini kwa Taifa hivyo wajumbe hao wana kazi kubwa ya kuisaidia Nchi kusonga mbele kutokana na maslahi mapana ya Nchi na kupelekea kusaidia adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuifungua Nchi kwenye uwekezaji.

Aidha ameagiza kuanza kwa vikao vya bodi mapema pamoja na vikao vya ziada ili kupitia mambo yote ambayo yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi kwa haraka ikiwemo kama kuna kampuni zinahitaji kuungana basi zisaidiwe kwa kufuata taratibu zote ili kusaidia upatikanaji wa ajira katika makampuni hayo kutokana na kuwepo kwa wimbi la ukosefu wa ajira.

Vilevile Dkt.Jafo amewataka wataalam wa taasisi hiyo kuwa mstari wa mbele katika kuisaidia na kuipa ushirikiano mkubwa Bodi hiyo kwani wao ndio injini katika utendaji ili kuipa kazi rahisi bodi hiyo kwa maslahi mapana ya Taifa.

Hata hivyo wakati akizungumza na watumishi wa Tume hiyo amewaasa kuishi kwa upendo na kufanya kazi kama timu moja ili kuliletea Taifa na Taasisi hiyo mafanikio.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani (FCC) Dkt. Aggrey Mlimuka amesema wameyapokea maelekezo hayo na kuahidi watayazingatia kwa kuyafanyia kazi ili kuleta matokeo chanya.

Dkt. Jafo amezindua Bodi hiyo baada ya kufanya uteuzi wa Wajumbe watatu (3) akiwemo Bw. Said Habibu Tunda, kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC,Prof. Jehovaness Aikael kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na CPA. Dkt. Shufaa M. Al-Beity kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).