Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali imepanga kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambapo kiasi cha Shilingi 600,000,000 zimetengwa.
Hayo ameyasema leo Julai 30,2022, Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifafanua mbele ya waandishi wa Habari majukumu ya Wizara na utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Dkt. Gwajima amesema Fedha hizo ni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali pamoja na mwanamke mjasiriamali mmoja mmoja.
Aidha Dkt. Gwajima amesema Katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali itaendelea kuhamasisha wanawake kujiunga katika majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.
“Majukwaa haya yapo kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa na Ngazi ya Taifa. Ili kuimarisha majukwaa haya, Wizara imepanga kutumia kiasi cha Shilingi 15,940,000 kusambaza Mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi pamoja na kuzindua Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.”
Dkt. Gwajima amesema, Serikali itaendelea kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
“Mwanamke ndiyo mlezi wa familia na jamii kwa ujumla, hivyo anahitaji kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili. Katika eneo hili, Wizara imetenga kiasi cha Shilingi 168,980,000. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote wakiwemo wadau wa maendeleo, asasi za kiraia, waandishi wa Habari na jamii kwa ujumla kwa kuwa jitihada za kumlinda mwanamke dhidi ya vitendo vya ukatili zinatakiwa kufanywa na kila mdau na kila mwananchi kwa nafasi yake.”
Pia Dkt. Gwajima amesema Wizara imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 45 kwa kundi la wafanyabishara ndogondogo maarufu kama machinga kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu katika masoko na kuwawezesha kupata mitaji ya kuendeleza biashara zao.
Amesema utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa Ushirikiano baina ya Wizara za kisekta zikiwemo; Ofisi ya Makamu wa Rais; Ofisi ya Waziri Mkuu; Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; OR-TAMISEMI; Uwekezaji, Viwanda na Biashara; Fedha na Mipango; Mambo ya Ndani ya Nchi; OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
Aidha amesema kuhusu maendeleo ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wizara imetenga Tsh. 5,300,000,000/= kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii.
“Fedha hiyo itatumika kuendelea kujenga na kukarabati mabweni, madarasa, kumbi za mihadhara, majengo ya utawala pamoja na Maktaba”. Amesema Waziri Gwajima.
Mbali na hayo Dkt. Gwajima amesema kwa mwaka 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi 508,254,000 kwa ajili ya kutekeleza shughuli ya usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo yanalenga kusaidia jamii katika afua mbalimbali zikiwemo elimu, afya, kilimo na utawala bora.
Dkt. Gwajima ameendelea kusema kuwa serikali itatekeleza ufanyikaji wa jukwaa la mwaka la NGOs linalotarajiwa kufanyika tarehe 28-30 Septemba, 2022 ambalo litatanguliwa na maazimisho yatakayofanyika katika ngazi za Halmashauri na Mikoa na kuhitimishwa katika ngazi ya Kitaifa. Pamoja na mambo mengine jukwaa linalenga kuunganisha wadau mbalimbali wa Maendeleo na Serikali.
Kuhusu malezi ya mtoto, Dkt. Gwajima amesema Wizara iko kwenye kuratibu uanzishaji wa vituo vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ambapo, kwa mwaka wa fedha 2021/22.
“Wizara imeanzisha vituo vya mfano vya malezi jumuishi 30 katika Mikoa ya Dodoma (20) na Dar es salaam (10). Katika vituo hivyo, 15 vimekamilika vyenye jumla ya watoto 883 (KE=467 na ME= 426). Katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 tunatarajia kufikia vituo 100 zaidi kwenye Mikoa 4.
Jumla ya Shilingi 383,750,000 zimetengwa ili kufanikisha kazi eneo hili.”
katika mwaka 2022/23, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Shilingi 32,310,981,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo, kati ya fedha hizo, Shilingi 18,169,057,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 14,141,924,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi. Kwa upande wa Shughuli za Maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi 11,092,080,000 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi 6,900,000,000 ni za mapato ya ndani na Shilingi 4,192,080,000 ni ufadhili wa wadau wa maendeleo toka nje ya nchi zikiwemo nchi rafiki, mashirika ya kimataifa na sekta mbalimbali zinazosaidia na kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best